Dondoo

Pasta mpenda sketi afichuliwa kwa ndoto

January 15th, 2019 1 min read

Na LEAH MAKENA

KAGEENE, MERU

MUUMINI wa kanisa moja eneo hili alijipata mashakani alipotimuliwa kanisani kwa kumwambia pasta kwamba aliota akiondolewa kama kiongozi wa kanisa hilo.

Yasemekana jamaa alimweleza pasta kwamba alifunuliwa ndotoni kwamba uongozi wake haungedumu kwa muda mrefu iwapo hangebadili mwenendo wake.

Kulingana na mdokezi, jamaa alimweleza pasta kwamba aliota akiwa amefumaniwa na wafuasi akistarehe na vichuna wa kanisa lake, jambo walilokashifu vikali na kumtaka kukoma kuongoza kanisa.

Muumini huyo alisema ndotoni alifunuliwa kwamba muda wa pasta kuhudumu ulikuwa ukikaribia kuisha kwa sababu ya tabia yake.

Mshiriki aliongeza kuwa ndoto hiyo ilikuwa na ukweli ndani yake akidai kuwa kila analoota huwa linatimia au kutimia baada ya muda na akamtaka pasta kutubu na kuomba ili kuepuka majaribu yaliyokuwa mbele yake.

Hapo ndipo pasta alipandwa na hasira na kuanza kumfokea muumini huyo akimtaja kama nabii wa shetani na kumtaka kutafuta kanisa tofauti ikiwa anaamini ni mbaya.

“Hata hauna haya kuja kwa mtumishi wa Mungu na kutoa hadithi za ujinga? Ninajua unaona gere kwa sababu vijana wananiheshimu na kuwa karibu na mimi ila sitakupa muda uendelee kupotosha washirika. Leo iwe mwisho wa kukuona kwenye uwanja huu,” pasta aliamuru.

Mfuasi alikubali kutii ila akaendelea kumuonya pasta kwenye mitandao ya kijamii akiwasihi washirika kutafuta makanisa mengine kwa madai kuwa pasta alikuwa amekosa maadili.

Minong’ono yasema kuwa pasta alikuwa mpenda vidosho na alifanya mipango kabambe nao chini ya maji na ndiposa akamfurusha jamaa kwa hofu kuwa njama zake zingegunduliwa.