Habari Mseto

Pasta muuaji aliwahi kufungwa Shimo la Tewa

January 9th, 2020 2 min read

DERICK LUVEGA na GASTONE VALUSI

PASTA aliyemuua mkewe kanisani kisha akajitoa uhai alikuwa ametumikia kifungo gerezani kwa kumtishia mkewe awali, imefichuka.

Mnamo Jumapili, Pasta Elisha Misiko wa Kanisa la Ground for God’s Gospel Ministries jijini Mombasa alimuua mkewe, Bi Ann Mghoi kwa kumdunga kisu kisha akajikata shingoni kwa kisu hicho wakati wa ibada.

Hapo jana, mamake Bw Misiko, Bi Margaret Nandoya alisema kuwa mzozo kuhusu usimamizi wa kanisa hilo ulianza baada ya mwanawe kumaliza kutumikia kifungo cha mwezi mmoja katika Gereza la Shimo la Tewa kwa shtaka la kutoa tishio la kumuua mkewe.

“Walitofautiana kuhusu umiliki wa kanisa hilo ambapo alimtumia mkewe jumbe za kumtishia. Mkewe aliripoti suala hilo kwa polisi. Hilo ndilo lilimfanya kukamatwa na kufungwa gerezani,” akasema Bi Nandoya nyumbani kwake Vihiga.

Akaongeza: “Wakati alipoondoka gerezani, alimpata mkewe akiliendesha kanisa hilo huku akichukua pesa zote zilizotolewa kama sadaka. Hilo ndilo lilimkasirisha.”

Bi Nandoya alisema kuwa mwanawe alifanya kazi za vibarua jijini Mombasa, hali iliyomwezesha kulijenga kanisa hilo bila usaidizi wowote.

Alisema kuwa alifahamishwa kuhusu mzozo huo, wakati suala hilo lilikuwa likiendelea kusuluhishwa.

“Alikuwa mtoto mzuri na mhubiri aliyeelewa kazi yake. Wawili hao walifanya harusi ya kanisa na wamekuwa wakitutembelea katika nyakati mbalimbali. Walikuwa na tofauti kadhaa kuhusu usimamizi wa kanisa hilo kwani walikuwa wakizozana kila wakati. Namwomba Mungu anisaidie. Sijui nitafanya nini. Nimesumbuka sana kutokana na tukio hilo,” akasema.

Bw Misiko alisomea katika Shule ya Msingi ya Chango, ambapo baadaye alielekea katika Shule ya Upili ya Mbale.

Mnamo Jumapili, aliondoka kutoka kiti chake na kumshambulia mkewe kwa visu viwili alivyokuwa ameficha katika shati lake.

Alimkata mara kadhaa. Washirika waliojawa na wasiwasi waliingilia kati na kumkimbiza katika Hospitali Kuu ya Pwani alikofariki alipokuwa akipokea matibabu.

Familia ya Bw Misiko, mwenye umri wa miaka 55, ilimtaja kuwa mtu aliyemcha Mungu na aliyejitolea kwa hali na mali maishani kulijenga kanisa hilo. Ilimlaumu mkewe kwa kuchukua usimamizi wake kwa nguvu.

Anatoka katika kijiji cha Idunga, Kaunti Ndogo ya Vihiga, Kaunti ya Vihiga, ambapo alikuwa kifungua mimba katika familia hiyo. Alilelewa katika Kanisa la Quakers lakini baadaye akabuni kanisa lake.

Wawili hao walikuwa wamewatembelea jamaa zao katika kaunti hiyo ambapo baadaye walirejea Mombasa. Wana watoto wanne.

Kwingineko, wanaume wameshauriwa kutafuta ushauri wanapohisi kuhangaishwa na wake zao ili wasaidiwe badala ya kuzua vurugu nyumbani.

Askofu wa kanisa la Missionary ya Kenya, Charles Kinyanjui alisema kuwa vifo vilivyotokea Jumapili kanisani Mombasa vingeepukwa endapo marehemu Misiko angetafuta ushauri wa wenzake na wataalamu.

“Nafikiri mambo kuhusu unyanyasaji na vurugu nyumbani hauchagui kama wewe ni mchungaji, mwanajeshi au mwalimu,” akasema katika afisi yake mjini Tala.

Bw Kinyanjui aliongeza kuwa wanaume huficha hisia zao zinazowapelekea kuwa na shida na mwishowe kuzua vurugu manyumbani mwao.

“Wanaume wanapaswa kufungua roho na kuongea waziwazi kuhusu masahibu yanayowazonga badala ya kunyamaa. Kama tungekuwa na wataalamu katika kila kijiji, mambo tangeimarika” akasema.

Wakenya wengi hutafuta huduma za ushauri kutoka kwa wachungaji.