Habari Mseto

Pasta ndani kuhubiri Huduma Namba ni ya kishetani

April 14th, 2019 2 min read

CHARLES LWANGA na CHARLES WASONGA

POLISI wa Malindi wamemkamata mhubiri mtatanishi Paul Makenzi kwa madai ya kuchochea wananchi dhidi ya kujisajili kwa mpango wa Huduma Namba.

Maafisa hao walimlaumu Bw Makenzi kwa kuwashauri wananchi kutoshiriki shughuli hiyo kupitia kipindi chake cha mahubiri kinachopeperushwa kupitia runinga ya Times TV. Anadaiwa kuwaambia watazamaji wa kipindi hicho kwamba nambari hiyo ni ya kishetani, na endapo watajisajili watakuwa wameuza nyoyo zao kwa shetani.

Katika kipindi hicho kwa jina, End Times, Bw Makenzi alifananisha Huduma Namba na zimwi linalozungumziwa katika Biblia, lenye alama ya kishetani ya nambari 666.

Wapelelezi na maafisa kutoka Bodi ya Kukagua na Kuorodhesha Filamu Nchini (KFCB) jana walivamia Kanisa lake kwa jina Good News International Church lililoko mjini Malindi na kuchukua kamera, kompyuta na santuri za DVD.

Meneja wa KFCB anayesimamia ukanda wa pwani Bonventure Kioko alisema maafisa wake walipata idhini ya mahakama ya kumzuilia Bw Makenzi katika kituo cha Polisi cha Malindi kwa siku 21 ili kutoa nafasi kwa polisi na wataalamu wa filamu kukamilisha uchunguzi.

Kumekuwa na tetesi kutoka kwa baadhi ya wananchi hasa viongozi wachache wa kidini, hata kabla ya shughuli hiyo kuanza, ya kuwepo kwa uhusiano kati ya Huduma Namba na nambari ya kishetani iliyozungumziwa katika kitabu cha Ufunuo katika Agano Jipya.

Hii ndiyo maana mnamo Aprili 2, Rais Uhuru Kenyatta alijitokeza waziwazi na kuwataka wananchi kupuuzilia mbali tetesi hizo akisema hazina ukweli wowote.

“Na wenzetu tusikubali kupotoshwa na wachache kuhusu Huduma Namba. Nilishangaa juzi kuwasikia makasisi wengi wakisema eti hii ni namba ya shetani. Kama Mkristo ninauliza, shetani ana uhusiano upi na shughuli ya kujiandikisha? Jameni tukome kueneza uwongo usio na maana,” Rais akasema alipoongoza hafla ya uzinduzi wa shughuli hiyo katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Masii, Kaunti ya Machakos

Rais alifafanua kuwa Huduma Namba ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuwawezesha wananchi kupata huduma kutoka serikali kwa njia rahisi.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka vile vile alipuuzilia mbali madai hayo alipoongoza shughuli hiyo katika kaunti ya Murang’a.

“Kama Mkristo aliokoka, ningependa kupinga kwa dhati dhana potovu zinazoeneza na watu fulani kuwa hii Huduma Namba ni ile nambari ya kishetani ya 666 inarejelewa katika Bibilia Takatifu. Hii ni nambari maalum ya kuwasaidia wananchi kupata huduma kwa haraka,” akasema.

Mnamo 2017 Bw Makenzi na mkewe Joyce Mwikamba walishtakiwa kwa kufundisha itikadi kali kupitia kanisa lao.

Shtaka lilisema kuwa wanandoa hao, kimakusudi, waliendeleza mafunzo ya itikadi kali katika kanisa lao liliko katika eneo la Furunzi.