Kimataifa

Pasta ndani miaka 15 kwa kubaka waumini 8 mara 40 kanisani

November 22nd, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

PASTA mmoja kutoka nchi ya Korea Kusini amehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani Alhamisi kwa kubaka waumini wanane katika zaidi ya mara 40 tofauti katika kanisa lake la Manmin Central Church jijini Seoul.

Shirika la habari la Yonhap linasema kwamba Lee Jae Rock, ambaye ni mwanzilishi wa kanisa hilo linaloaminika kuwa wafuasi takriban 130,000, alihukumiwa katika mahakama ya Seoul Central District Court kwa kutumia mamlaka yake kutenda uovu huo.

Pasta huyo mwenye umri wa miaka 75 alitumia imani ambayo ‘kondoo’ hao walikuwa nayo kwake kama mtu aliyekuwa karibu na Mungu, kuwadhulumu mara kwa mara.

Kanisa hilo, ambalo lilianzishwa na Lee mwaka 1982 na linadai kuwa na zaidi ya matawi 10,000 kote duniani, ikiwemo Kenya, liliondolewa kutoka orodha ya Baraza la Makanisa la Korea mwaka 1999 kutokana na madai linaenda kinyume na maandiko ya Kikristu.

Katika tovuti yake, kanisa hilo linadai kuwa “idadi kubwa ya watu isiyojulikana imepata uponyaji wa Mungu kwa magonjwa yasiyotibika kama Ukimwi, saratani, na mengineyo, mara moja.