HabariSiasa

Pata potea ya nyumba nafuu

April 25th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

MATUMAINI ya Wakenya watakaokatwa pesa kwenye mishahara yao kufadhili ujenzi wa nyumba nafuu chini ya mpango wa serikali wa Ajenda Nne yaliyeyuka jana baada ya kubainika kwamba umiliki wa nyumba hizo utakuwa jambo la bahati nasibu.

Katibu katika Wizara ya Ujenzi anayehusika na miundomsingi, Bw Charles Hinga, alisema watakaobahatika kuzipata ni wale watakaochaguliwa kwa mfumo wa pata potea.

Kulingana na serikali, licha ya kuwa wafanyakazi wote wasio wa ‘jua kali’ watakatwa asilimia 1.5 ya mishahara kwa lazima kufadhili ujenzi huo, wafanyakazi kama hao watalazimika kutuma maombi, kukaguliwa kisha kushindana ili atakayebahatika apokezwe nyumba hiyo.

Serikali inalenga kujenga nyumba 500,000 katika kipindi cha miaka mitatu na nusu, ingawa jumla ya wafanyakazi milioni tatu watakuwa wakikatwa pesa, pamoja na watakaojitolea kwa hiari.

Akizungumza Jumanne usiku, Bw Hinga alifichua kuwa utaratibu wa bahati nasibu utatumiwa kuamua watakaomiliki nyumba hizo.

“Sharti mtu ajisajili kando na kuchanga pesa, kabla apewe nyumba. Mfumo wa pata potea utatumiwa kuamua watakaopata nyumba husika. Atakayeangukiwa na bahati, ndiye atakayeuziwa,” Bw Hinga akasema, akihojiwa kwenye runinga ya Citizen.

Katibu huyo alisema, kwa kuwa Wakenya walichagua serikali ya Jubilee ni vyema pia wawe tayari kukatwa pesa, kwa kuwa ni sehemu ya manifesto ya serikali.

Aliwaambia wale ambao tayari wanamiliki nyumba, ama ambao wamekopa ili kununua nyumba kupitia mipango mingine kuwa tayari kukatwa pesa hizo vilevile. Ina maana kuwa hata mtu akiwa tayari analipa mkopo wa kujenga nyumba, atalipa pesa za kujenga nyumba hizo za serikali.

Maelezo yake, hata hivyo, yaliwaacha Wakenya wengi na ghadhabu, wakilalamika kuwa mradi huo una njama fiche na kuwa, kuna uwezekano mkubwa kuwa pesa za wananchi zitaporwa.

Wakenya wameshangazwa na nia ya kuwatoza pesa kwa lazima, kisha kutumia mfumo wa pata potea kugawa nyumba hizo.

“Mfumo wa Kamari? Nikatwe mshahara ili nyumba ijengwe, kisha nikashindane kwa njia ya kubahatisha ambapo najua nitashindwa. Mungu aingilie kati,” akasema Reuben Zia.

Wengi waliendesha kampeni dhidi ya mpango huo kwa mara nyingine kwenye mitandao ya kijamii, wakisema hawautaki.

“Wazo kuhusu ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ni lenye umuhimu mkubwa lakini ulafi, ufisadi na maono yasiyo na mwelekeo yameliharibu kuanzia mwanzo,” akasema Sam Kaunda.

Wakenya wamekuwa wakikosoa jinsi mpango huo unalenga kuendeshwa pamoja na mapengo mengine kisheria na kimuundo, na sasa hali ya wafanyakazi wanaochangia kutokuwa na uhakikka wa kumiliki nyumba hizo imewatamausha wengi hata zaidi.