Makala

PATA USHAURI: Athari za maziwa ya poda na yale ya ng’ombe kwa watoto wachanga

July 30th, 2019 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

KULINGANA na Shirika la Afya Duniani (WHO), protini na jumla ya kiwango cha matumizi ya nishati mwilini, vilevile kiwango cha nishati inayovunjwavunjwa, kiko juu miongoni mwa watoto wachanga wanaonyweshwa maziwa ya poda, ikilinganishwa na wanaonyonyeshwa.

Tofauti katika kuzalisha insulini (homoni inayohusika katika kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu) na homoni zingine kwenye kongosho na utumbo, pia zilishuhudiwa baina ya watoto wanaonyonyeshwa na wanaonyweshwa maziwa ya poda.

Aidha unyweshaji wa maziwa ya poda husababisha viwango vya juu vya plazma kwenye insulini, ambavyo kwa upande mwingine huchochea uzalishaji mafuta na ukuaji mapema wa seli zinazohifadhi mafuta (adipocytes).

Wataalamu wa masuala ya lishe wanasema kwamba maziwa ya ng’ombe na yale ya poda ya watoto wachanga yana viwango vya juu vya mafuta na kabohaidreti, suala ambalo huenda likasababisha matatizo ya uzani mkubwa.

Viwango hivi vya juu vya virutubisho hivi vinasemekana huenda vikasababisha kuongezeka kwa uzani.

Kadhalika mafuta zaidi kwenye maziwa ya ng’ombe na hayo ya poda yamegunduliwa kuwa kichocheo cha maradhi ya kisukari.

Ugumu

Aidha, yanaweza ongeza idadi ya seli za mafuta mwilini au kuzidisha chembechembe za mafuta katika seli za mwili, na hivyo kufanya vigumu kwa insulini kufyonzwa.

Haya ni mambo yanayoshuhudiwa mtu anapougua maradhi ya kisukari ya type 2 (type 2 diabetes), sawa na inavyokuwa mtoto anapokumbwa na maradhi ya kisukari ya Type 1 (type 1 diabetes), mwili unapozalisha kiwango kidogo au kukosa kabisa kuzalisha insulini.

Katika hali hii, wazazi hulazimika kuwalisha watoto wao chakula kingi ili kuimarisha kiwango cha sukari kwenye damu, ambapo kwa upande mwingine chakula hiki husababisha watoto hawa kukumbwa na tatizo la uzani mzito.

Ili kukabiliana na tatizo hili, wazazi wanashauriwa kuwalisha watoto wao (hasa wanaotambulishwa kwa chakula kwa mara ya kwanza), mboga na matunda.

Uzani mzito umehusishwa na maradhi mbalimbali ya moyo kama vile kiharusi na hata kusitisha shughuli za baadhi ya viungo mwilini.