Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Je, naugua 'ugonjwa' wa wasiwasi au akili?

August 25th, 2020 3 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Tangu utotoni nimekuwa mtu mwenye wasiwasi. Hata hivyo, katika kipindi cha miezi michache sasa, mawazo yamekuwa mengi hata zaidi. Mbali na kukumbwa na hofu ya kutemwa na mpenzi wangu, wasiwasi kuhusu taaluma yangu, vile vile hisia za kwamba huenda nikawapoteza wapendwa wanikaba. Hofu yangu imekuwa nyingi sana hadi nimeanza kuwachosha wanipendao. Ni hali ambayo pia imenisababishia madhara ya kimwili ikiwa ni pamoja na kukosa usingizi, maumivu ya kifua na matatizo ya kupumua. Je, ni ugonjwa wa wasiwasi au akili? Tafadhali nahitaji usaidizi wa dharura.

Jessy, Nairobi

Mpendwa Jessy,

Unawaza sana na unakumbwa na matatizo ya kiakili yanayofahamika kama anxiety disorder. Hali hii hutokea mwili unapojaribu kukabiliana na msongo wa akili, hofu au fikra. Hii inapofanyika, mwili unajiandaa kukabiliana na au kuepuka kichocheo.

Wakati huu, mwili hutoa homoni kama vile adrenaline na cortisol ambazo zinaongeza mpigo wa moyo, kasi ya kupumua, kiwango cha glukosi kwenye damu, kiwango cha mzunguko wa damu katika ubongo na misuli, na kupunguza mzunguko wa damu katika mfumo wa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Haya yote hufanyika kukusaidia kukabiliana na vichocheo hivi.

Unapokumbwa na hali hii, mbali na kukumbwa na hofu na wasiwasi, pia kuna athari za kimwili kwa sababu uwezo wa mwili kukabiliana na msongo wa mawazo haujasawazishwa. Hii ndio sababu unakumbwa na matatizo ya kulala, maumivu ya kifua na matatizo ya kupumua.

Unashauriwa kumuona daktari wa akili au mwanasaikolojia. Baada ya kufanyiwa uchunguzi utapewa dawa ya kukusaidia kupunguza wasiwasi na msongo wa akili.

Itakuwa vyema ikiwa utapitia utaratibu wa tiba ya kiakili kwa usaidizi wa mwanasaikolojia, ili kujifunza mbinu za kukusaidia kutulia na jinsi ya kudhibiti masongo wa mawazo na wasiwasi.

Litakuwa jambo zuri ikiwa utaandika kinachokupa wasiwasi, yaani kiini cha wasiwasi, nini hasa kinachosababisha, kisha uchague suluhu muafaka na ujitahidi kuitekeleza.

Mpendwa Daktari,

Nitakabiliana vipi na upele unaojitokeza katika sehemu zangu za siri kila ninapoondolewa nywele kwa mbinu ya ‘waxing’?

Maryanne, Mombasa

Mpendwa Maryanne,

Hali inayokukumba inafahamika kama pseudo-folliculitis. Baada ya kunyoa, nywele zinapoota upya zinaingia kwenye ngozi kupitia vinyweleo au ncha kali za nywele zinadunga vinyweleo vya ngozi kabla ya hata nywele kuota na kuchomoka nje.

Hii husababisha mwasho na sehemu hiyo kuvimba na kugeuka nyekundu. Kuna wakati ambapo sehemu hii yaweza kumbwa na maambukizi na kusababisha uvimbe zaidi, uchungu na hata usaha. Hii yaweza tokea popote ambapo nywele zimenyolewa au kung’olewa ikiwa ni pamoja na uso, makwapa, kinena na miguu.

Ni hali inayokumba sana watu walio na nywele zilizojisokota ikilinganishwa na watu walio na nywele zilizonyooka. Aidha, tatizo hili huwakumba sana wanaume wa asili ya Kiafrika, lakini pia yaweza wakumba wanawake.

Tiba sahili ni kuacha nywele ziote na kuzichenga, badala ya kuzinyoa zote. Nywele zilizoota ndani ya ngozi zaweza ondolewa kwa kutumia kikoleo. Kuna baadhi ya krimu ambazo zaweza tumika kusaidia kupunguza uvimbe na maambukizi.

Ili kuzuia uvimbe unaotokana na kunyoa nywele kwa kutumia wembe:

• usinyoe nywele zako kila siku; ruka angaa – angalau – siku moja

• unaponyoa, acha angaa nywele za urefu wa kati ya milimeta 0.5 na milimeta 1 badala ya kuzinyoa zote

• tumia kifaa cha wembe mmoja ili kuzuia kunyoa karibu sana na ngozi

• tumia wembe wa kielektroniki ambapo baadaye lazima usafishwe na kutibiwa vilivyo

• nyoa kwa mwelekeo wa vinyweleo na wala sio dhidi yake na wala usinyoshe ngozi

• fanya nywele ziwe nyepesi kwanza kwa kutumia kitambaa kilicholoweshwa majini au nyoa ukiwa unaoga kwa maji moto

• bambua ngozi ya sehemu hii na kuipaka mafuta kwa mfano kwa kutumia bidhaa kama vile glycolic acid peel (inayoundwa kutokana na mua)

• nyoa nywele kwa kutumia kemikali, kwa mfano barium sulfide paste

• tumia mbinu za kudumu za kuondoa nywele kwa mfano kwa kutumia laser au electrolysis, Vaniqa cream (eflornithine hydrochloride 13.9%)