Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Jicho la kulia latetema

February 4th, 2020 2 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

KWA wiki kadhaa sasa, jicho langu la kulia limekuwa likitetema. Je, kuna maelezo ya kimatibabu kuhusu tatizo hili au niamini tu nadharia ya kishirikina ambayo nimekuwa nikisikia kutoka kwa marafiki zangu?

Jenn, Nairobi

Mpendwa Jenn,

Mtetemo wa kigubiko cha jicho husababishwa na mnyweo wa misuli katika sehemu hii. Mara nyingi hali hii haisababishi matatizo mengi na mambo hurejea kawaida baada ya muda bila matibabu, japo huenda tatizo hili likarejea baadaye. Wakati mwingine hakuna sababu ya mtetemo huu. Kuna wakati mwingine ambapo huenda hali hii ikatokana na maumivu ya kichwa, mwasho au jeraha la macho, macho makavu, mzio wa macho, kukosa usingizi, uchovu, mfadhaiko, uvutaji sigara, unywaji pombe au kafeini, kuwa wazi kwa upepo au kutokana na matumizi ya dawa fulani. Hata hivyo ni nadra kwa mtetemo wa jicho kusababishwa na tatizo la neva. Hii yaweza kutokea ikiwa mtetemo huu utadumu kwa muda mrefu na ikiwa ni mkali sana na unaathiri vigubiko vya macho; ikiwa tatizo hili linasababisha maumivu, au ikiwa sehemu zingine za uso pia zimeathirika. Endapo unashuku kwamba una jeraha la macho, sehemu zingine za uso zimeathirika, au mtetemo huu utaendelea kwa muda mrefu, tafadhali muone daktari.

 

Mpendwa Daktari,

Nimekuwa nikipata upele baada ya kuondoa nywele za nyeti kwa kutumia mbinu ya ‘waxing’. Sababu yaweza kuwa nini?

Nicky, Mombasa

Mpendwa Nicky,

Baada ya kuondolewa nywele za nyeti kupitia utaratibu wa ‘waxing’ au kunyoa, nywele zinapoota tena ncha zake kali hupenyeza vinyweleo vya ngozi kabla ya kuchomoza nje na kuonekana. Hii husababisha sehemu hiyo kuvimba na kuwa nyekundu. Hali hii inaitwa ‘pseudo-folliculitis’. Wakati mwingine sehemu hii yaweza pata maambukizi. Hii yaweza kuathiri sehemu yoyote ambapo nywele imeondolewa kwa utaratibu wa ‘waxing’ au kunyolewa kwa wembe ikiwa ni pamoja na usoni, makwapa, nyeti na hata miguuni.

Tiba sahili ni kuacha nywele hizi kuota au kuzichanja badala ya kuziondoa kabisa. Unaweza kutumia krimu za kuondoa nywele au kufanyiwa utaratibu wa kudumu wa kuondoa nywele kama vile ‘laser’ au ‘electrolysis’. Uvimbe unaotokana na nywele zilizoota ndani za ngozi waweza kuondolewa kwa utaratibu kwa kutumia kikoleo. Kuna baadhi ya krimu ambazo hutumiwa kupunguza uvimbe huu. Ikiwa kuna maambukizi, utahitaji viua vijasumu.

 

Mpendwa Daktari,

Nimekuwa nikikumbwa na mzio kila ninapoenda kuogelea. Kwa kawaida mimi hupata mafua, hali inayoandamana na kidonda kwenye mdomo. Tatizo laweza kuwa nini?

Jerry, Mombasa

Mpendwa Jerry,

Vidimbwi vya kuogelea huongezwa klorini ili kuua bakteria na kupunguza maambukizi ya maradhi. Hata hivyo, klorini ina uwezo wa kusababisha mwasho kwa ngozi, macho na mfumo wa kupumua. Aidha, klorini yaweza kusababisha upele, macho kuwa mekundu, kutokwa na kamasi na matatizo ya kupumua. Mambo yaweza kuwa mabaya hata zaidi kwa watu ambao tayari wana mzio wa chavua, vumbi, baridi na kadhalika. Unaweza kudhibiti hali kwa kupunguza muda unaotumia kidimbwini. Waweza pia kutumia vidimbwi vilivyo nje ya majengo badala ya vilivyo ndani, jiepushe na vidimbwi vilivyo na viwango vingi vya klorini. Pia waweza kuwa na mazoea ya kuoga pindi baada ya kuogelea na kutumia dawa za kukabiliana na mzio kabla na baada ya kuogelea. Aidha, waweza kutumia kibano cha pua unapoogelea. Mara nyingi hali hii huisha yenyewe baada ya muda au waweza kutumia dawa za kukabiliana na virusi ili kupunguza muda ambao kidonda kitadumu, na pia kuzuia tatizo hili kutokea kila mara.