Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Jipu kubwa sehemu nyeti chungu sana

July 30th, 2019 2 min read

DKT FLO

NINA umri wa miaka 26. Nina chunusi kubwa, au jipu ambalo limekuwa likijitokeza katika sehemu yangu nyeti kila ninapokaribia hedhi. Ni chungu sana na huisha hedhi inapokaribia kuisha. Lakini wakati huu mambo yamekuwa tofauti kwani limekaa kwa takriban miezi miwili sasa bila mabadiliko ambapo ni chungu, limevimba na linanitatiza. Shida ni nini, na nifanyeje tafadhali?

Fatma, Nairobi

 

Mpendwa Fatma,

Uvimbe unaojitokeza kila mara kwenye nyeti au makwapani hujitokeza vinyweleo vya nywele (nywele zinakochomoza kutoka kwa ngozi) zinapozibwa na bakteria na vitu vingine. Kuna baadhi ya watu ambao hukumbwa na wasiwasi vinyweleo vyao vinapozibwa pengine kutokana na kinga mwili dhaifu au kwa sababu ya mabadiliko ya kihomoni kama vile mambo yanavyoshuhudiwa wakati wa hedhi. Tatizo hili aidha, huwakumba watu wenye uzani mzito. Haliambukizwi wala kusababishwi na viwango duni vya uchafu. Wakati mwingine uvimbe huu huisha kivyao na huenda ukaacha kovu. Kwa upande wako ambapo uvimbe huu umekuwa kwa wiki kadha, unahitaji kumuona daktari au mtaalam wa ngozi ili upewe viua vijasumu na dawa za maumivu. Mtaalamu wa ngozi atakufahamisha iwapo unahitaji matibabu zaidi.

******

Daktari,

Nimekuwa nikikumbwa na maumivu ya mgongo kwa takriban miezi miwili. Uchungu huu huzidi baada ya siku nzima ya kufanya kazi afisini. Ninapomeza dawa za kukabiliana na maumivu, shida hii hutokomea kwa siku moja au mbili na kurejea tena. Je, yaweza kuwa kwa sababu ya kiti ninachokalia kazini? Kiti hiki hakina starehe na mimi hukikalia kwa masaa mengi kila siku. Tafadhali nisaidie.

Ken

 

Mpendwa Ken,

Yawezekana kwamba maumivu ya mgongo unayokumbana nayo ni kutokana na kuketi kwa muda wa saa nyingi kila siku kwenye kiti kishicho na starehe. Huenda pia hautumii mkao mzuri. Unapaswa kuketi mgongo ukiwa wima, digrii 90 kwa mapaja yako, ambayo pia yanapaswa kuwa digrii 90 kwa miguu yako. Viwiko vyako vinapaswa kuwa juu ya meza kiwango sawa na kifua chako, na ikiwa unatumia kompyuta, inapaswa kuwa kiwango kinachoambatana na macho yako, takribani sentimeta 30 kutoka kwako. Usijipinde unapoandika kwa kutumia kompyuta. Unapaswa kukaa wima hata unapotazama televisheni na pia usimame wima na kutembea vivyo hivyo. Usikae kwa muda mrefu zaidi ya dakika 45 bila kusimama na kutembea. Jaribu kufanya kazi ukiwa umesimama kwa dakika chache. Iwapo maumivu yatazidi, kuna dawa za maumivu na krimu za kutuliza misuli ambazo zaweza kutumika, vile vile mafuta ya kukanda mgongo. Tibamaungo pia yaweza kusaidia na unaweza kufunzwa mazoezi ambayo waweza kujifanyia mwenyewe.

******

Mpendwa Daktari,

Mamangu amekuwa akitumia dawa yza maradhi ya kisukari aina ya Type 2 (type 2 diabetes) kwa zaidi ya miaka kumi, na nilisoma mahali kwamba mchanganyiko wa mdalasini na juisi ya mboga waweza kuponya kisukari. Kwa nini madaktari hawatupi suluhu hizi za kiasili huku wakizidi kutupendekezea dawa zile zile kila wakati?

Mwanawe, Omari

 

Mpendwa Omari,

Kisukari aina ya Type 2 (Type 2 diabetes) huanza mfumo unaokabiliana na sukari mwilini unapodinda kufanya kazi. Ni hali ambayo huendelea muda unavyozidi kusonga, na pindi mfumo huu unapofeli kabisa, hali ya kawaida haiwezi kurejeshwa. Dawa husaidia mwili kukabiliana na sukari na iwapo matumizi yatasitishwa au kuendelea kinyume na mwongozo wa daktari, kiwango cha sukari kwenye damu kitaongezeka na kusababisha matatizo mengine kama vile figo kusitisha shughuli, suala ambalo laweza kusababisha upofu. Kuna matibabu mengine mbadala ambayo yamependekezwa. Mengine hayajahimiliwa kisayansi na hivyo sio jambo la busara kuyafuata.