PATA USHAURI WA DKT FLO: Kiharusi cha muda huletwa na nini?

PATA USHAURI WA DKT FLO: Kiharusi cha muda huletwa na nini?

Mpendwa Daktari,

Nini kinaweza sababisha kiharusi cha muda mfupi (mini-stroke) kwa mtu ambaye hajatimu umri wa miaka 50?

R.K, Nairobi

Mpendwa R.K,

Kwa lugha ya kitaalamu hali hii inafahamika kama shambulio la Transient Ischaemic Attack (TIA), ambapo damu inazuiwa kwa muda na kukosa kufikia sehemu ya ubongo, uti wa mgongo au sehemu ya nyuma ya jicho (retina). Hii husababisha jeraha kwa tishu iliyoathirika na mara nyingi, mgonjwa atapata nafuu kabisa. Hata hivyo, kukumbwa na kiharusi hiki kunamaanisha kwamba kuna uwezekano kwa mhusika kupata kiharusi kamili.

Kuziba kwa mishipa ya damu kunatokana na kuganda kwa damu, mishipa ya damu kuwa miembamba kutokana na uchafu, hali ambayo huenda ikasababishwa na maradhi ya kisukari, viwango vya juu vya cholesterol au kuvuta sigara. Ili kuzuia kutokea kwa visa hivi katika siku zijazo, kinachosababisha hali hii kinapaswa kutambuliwa na kutibiwa. Kwa mfano matumizi ya dawa za kuzuia damu kuganda, shinikizo la moyo, kisukari na kudhibiti viwango vya cholesterol.

Aidha, dumisha lishe bora na ule kwa wingi vyakula vilivyo na viwango vya juu vya mboga na matunda.

Nitakabiliana vipi na hedhi nyingi kupindukia?

Jano, Mombasa

Mpendwa Jano,

Hali hii inayofahamika kwa Kiingereza kama heavy Menstrual Bleeding (HMB) hutokea iwapo mwanamke atavuja damu zaidi ya milimita 80 baada ya siku kadha za hedhi.

Ni hali ambayo iwapo haitakabiliwa huenda ikamsababishia mhusika maradhi ya anemia.

Iwapo utavuja damu kwa zaidi ya wiki moja, kulowesha kitanda kwa damu au ikiwa utalazimika kutumia zaidi ya visodo sita kwa siku, basi huenda unakumbwa na hali hii. Unasemekana unakumbwa na hali hii ikiwa utalazimika kutumia visodo vingi kupindukia na kubadilisha baada ya masaa mawili; itakubidi uvalie nepi za watu wazima ili kukabiliana na damu nyingi inayovuja; utatokwa na hedhi kwa zaidi ya siku saba; utatoka damu nyingi hasa unaposimama; utalazimika kutoenda kazini au kutohudhuria hafla zingine za kijamii kwa sababu ya kutokwa na damu nyingi kupindukia au iwapo utashuhudia hedhi baada ya chini ya siku 28 au baada ya zaidi ya siku 35.

Ishara zingine za kuzingatiwa ni uchungu, uchovu, kisunzi na homa.

Hali hii husababishwa na kutokuwa na usawa wa homoni mwilini. Estrogen na progesterone ni aina mbili za homoni zinazohusika na hedhi. Iwapo hakutakuwa na usawa baina ya homoni hizi mbili, basi huenda tatizo hili likatokea.

Matumizi ya baadhi ya mbinu za upangaji uzazi zinazohusisha kuingizwa kifaa kwenye uterasi, matatizo ya ujauzito, maambukizi katika sehemu za uzazi, japo sio kawaida, kuna aina za kansa kama vile ya njia ya uzazi, uke na ovari zinazoweza sababisha hali hii. Kila mara unapogundua kuwa unavuja damu kupindukia wakati wa hedhi, sharti utafute matibabu.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Jinsi ya kukabiliana na kiharusi cha muda...

KWA KIFUPI: Chanjo ya kukabiliana na aina mpya ya corona...