Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Koili husababisha maumivu tumboni

September 10th, 2019 3 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Natumia kitanzi cha kuzuia mimba (Intra-uterine Device) kama mbinu ya kupanga uzazi. Katika kipindi cha miaka minne, kifaa hiki kimenifaa sana, lakini hivi majuzi nimekuwa nikikumbwa na maumivu makali katika sehemu ya chini ya tumbo langu, vile vile maumivu makali kwenye wayo zangu. Nashuku kwamba huenda kifaa hiki kimesonga na ndicho kinanisababishia matatizo haya. Je, nimekosea?

Mwanamke mwenye wasiwasi

Mpendwa,

Kitanzi au ukipenda IUD (Intra-uterine Device) au koili yaweza kusonga na kusababisha maumivu makali na kuvuja damu nyingi. Ili kuangalia mkao wa kifaa hiki, tafadhali nenda ukaguliwe na mwanajinakolojia ambapo pia utapigwa picha ya ultrasound scan. Ikiwa hilo ndilo tatizo, yaweza kurejeshwa katika sehemu inayofaa au hata kuondolewa. Mwanajinakolojia aidha, atakukagua kubaini ikiwa una matatizo mengine yanayosababisha maumivu ya tumbo kama vile shida ya mfumo wa uzazi au wa kupitisha mkojo, au hata tatizo la utumbo.

Tatizo kwenye nyayo zako ni shida tofauti ambapo yaweza kuwa kuvimba kwa tishu nyepesi katika sehemu hii. Tatizo hili hutokea hasa ukiwa na uzani mzito, au ikiwa wewe husimama au kutembea kwa muda mrefu, au ikiwa wayo zako ni bapa au endapo utao wa mguu wako uko juu (high foot arch). Kuvalia viatu visivyo himili vyema tao za miguu yako pia huchangia tatizo hili.

Ili kukabiliana na tatizo hili, kabiliana na shinikizo kwa miguu yako kwa kupunguza muda unaochukua kusimama au kutembea. Pia, unaweza kufanya mazoea ya kujinyoosha na kukanda miguu yako kabla ya kuondoka kitandani. Valia viatu vinavyohimili vyema tao za miguu yako na vilivyo na visigino tulivu au vilivyoinuka kidogo. Aidha, dawa za kukabiliana na maumivu zitapunguza uchungu na uvimbe kwenye sehemu hii.

 

Mpendwa Daktari,

Ningependa kujua ishara za mapema za kansa ya lango la uzazi.

Martha, Mombasa

Mpendwa Martha,

Kwa bahati mbaya, hakuna ishara za mapema za maradhi haya. Pindi unapoanza kushuhudia ishara, maradhi haya huwa yamesambaa. Ishara ni pamoja na kutokwa na damu baada ya kushiriki tendo la ndoa, kuvuja damu katikati ya siku zako za hedhi au kutokwa na damu baada ya kukatikiwa; majimaji yenye chembechembe za damu na harufu mbaya, maumivu makali sehemu ya chini ya tumbo unaposhiriki tendo la ndoa. Mbinu ya kipekee ya kunasa kansa ya mlango wa uzazi ni kwa kufanyiwa uchunguzi kila mara wa iwapo kuna seli za kansa (pap smear) na /au kufanyiwa uchunguzi wa HPV-DNA. Ikiwa matokeo baada ya uchunguzi huu yataonekana kutokuwa ya kawaida, uchunguzi zaidi utafanywa, kwa mfano uchunguzi wa lango la uzazi (colposcopy) na seli au tishu zilizozingira sehemu hii(biopsy), kisha uchunguzi zaidi na matibabu endapo matokeo yatathibitisha kuna haja.

 

Mpendwa Daktari,

Kwa wiki moja sasa nimekuwa nikikumbwa na malengelenge katika sehemu inayozingira uume wangu, na nina wasiwasi kwamba huenda hivi vikawa vidutu vya sehemu nyeti (genital warts). Nifanyeje?

Musa, Kakamega

Mpendwa Musa,

Malengelenge katika sehemu inayozingira nyeti zako yaweza kuwa kutokana na maambukizi ya Herpes au ya bakteria.

Pia, yaweza kutokana na vidutu vya nyeti ambavyo husababishwa na maambukizi ya virusi vya Human Papilloma Virus (HPV), maradhi ya zinaa ambayo yamekithiri.

Vidutu hivi huathiri sehemu nyeti na tupu ya nyuma.

Kwa kawaida vidutu hivi huanza kama uvimbe mdogo na vyaweza kuota na kuwa vikubwa kiasi cha kufanana na koliflawa.

Unaweza kuambukizwa HPV kutokana na mgusano wakati wa ngono au kutokana na mgusano wa ngozi na mtu aliyeambukizwa. Kwa watu wengine, vidutu hivi havina maumivu, lakini huenda ukakumbwa na mwasho, kuvuja damu au kutokwa na maji maji.

Ni muhimu kufanyiwa uchunguzi na daktari ili ajue kiini kamili cha tatizo linalokukumba. Ikiwa malengelenge hayo yanatokana na maambukizi ya bakteria, basi utapewa viua vijasumu.

Ikiwa ni kutokana na maambukizi ya Herpes, utapewa dawa za kukabiliana na virusi. Ikiwa unakumbwa na vidutu vya nyeti, daktari atakupendekezea krimu kama vile imiquimod, podophylin, trichlorocetic acid, na matibabu mengine kama vile cryotherapy, electrocautery, laser treatment au upasuaji.

Baada ya matibabu, huenda vidutu hivi vikajitokeza tena kwani tiba hii inaweza kupunguza makali mwilini kwa muda, kisha virusi vya HPV kujitokeza tena.

Ili kuzuia maambukizi mapya au kusambaza maambukizi haya, shiriki tendo la ndoa kwa kutumia kinga (kondomu), kuwa mwaminifu kwa mpenzi mmoja ambaye hajaambukizwa au usishiriki ngono kabisa.