Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Maumivu kooni yanitia wasiwasi

September 17th, 2019 2 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Nimekuwa nikikumbwa na maumivu ya koo kwa miezi miwili sasa. Licha ya kwamba nimekuwa nikipokea matibabu, sijashuhudia mabadiliko. Je, hii yaweza kuwa dalili ya kansa ya koo?

Mkazi wa Nairobi

Mpendwa,

Kukumbwa na maumivu ya koo kwa mwezi mmoja yaweza kutokana na maambukizi ambayo hayajatibiwa. Aidha, hii yaweza kutokana na mwasho unaosababishwa na kamasi puani au ‘sinusitis’ inayosababisha kutiririka kwa kamasi kwenye koo pengine kutokana na mzio au maambukizi ya uwazi katika mfupa (hasa ndani ya fuvu) unaowasiliana na mianzi ya pua (sinus). Maumivu ya koo pia yaweza kuwa kutokana na chakula tumboni kupanda juu hadi kwenye umio (oesophagus), na hivyo kusababisha mwasho katika sehemu hii, na wakati mwingine kuenda hadi kwenye njia ya kupitisha hewa. Kukaukiwa, kutaabika kutoa sauti, kukohoa kwa muda mrefu na kusafisha koo, aidha ni baadhi ya mambo ambayo yaweza kusababisha maumivu ya koo.

Unashauriwa kutafuta ushauri wa mtaalamu wa ENT ili ufanyiwe uchunguzi wa koo. Matibabu yatategemea na kinachosababisha tatizo lako, kwa mfano, mzio unatibiwa kwa kutumia anti-histamines, viua vijasumu hupendekezwa kutibu maambukizi yoyote, dawa maalum ya kunyunyiza puani (nasal spray) yaweza kutumika kuzibua uwazi katika mfupa unaowasiliana na mianzi ya pua na vilevile dawa za kupunguza viwango vya asidi tumboni. Aidha, kunywa kati ya glasi 6 na 8 za maji ili kuepuka tatizo la kutaabika kutoa sauti, vile vile kusafisha koo lako kila mara.

 

Mpendwa Daktari,

Ni mara ngapi mtu anapaswa kutumia tembe za dharura za kupanga uzazi (E-Pill) ?

Mwanaisha, Mombasa

Mpendwa Mwanaisha,

Tembe za dharura za kupanga uzazi zinapaswa kumezwa katika kipindi cha muda wa saa 120 baada ya kushiriki tendo la mahaba bila kinga, iwapo una wasiwasi kwamba mbinu ya uzazi unayotumia imefeli kufanya kazi, au baada ya kudhulumiwa kimapenzi. Kuna tembe zinazomezwa mara moja na zingine humezwa mara mbili, au unaweza kuwekewa kitanzi cha kuzuia mimba (intra-uterine device), kifaa ambacho husalia kwa miaka kadha. Ikiwa unalazimika kutumia tembe za dharura kila siku, basi unashauriwa kutumia mbinu ya kupanga uzazi ya kudumu ili kuepuka tatizo la mbinu hii kufeli kufanya kazi, au kuzuia kukumbwa na athari zinazotokana na matumizi ya kila wakati ya tembe hizi za dharura.

 

Mpendwa Daktari,

Rafiki yangu amekuwa akikohoa kwa miezi sasa. Nashuku kwamba ni kifua kikuu (TB). Kama marafiki, vile vile familia yake tutajiepushaje na maradhi haya pasipo kumfanya ahisi kwamba tunamtenga?

Gracy

Mpendwa Gracy,

Ishara kamili ya kifua kikuu (TB) ni kikohozi kinachoendelea kwa zaidi ya wiki mbili, homa kali, kutokwa na jasho jingi wakati wa usiku na kupunguza uzani. Mgonjwa atahisi mdhaifu na mchovu na huenda kikohozi kikatoka kikiwa kimechanganyika na chembechembe za damu au kuvimba kwa tezi za limfu (lymph nodes). Yeyote anayezidi kukohoa kwa zaidi ya majuma mawili hasa baada ya kupokea matibabu, anapaswa kupimwa kubaini iwapo anaugua (TB) ambapo uchunguzi hufanyiwa kikohozi chake na hata mhusika kupigwa picha za X-ray kifuani. Pindi baada ya matokeo kujulikana, kuna dawa thabiti za kutibu TB, pasipo kuzingatia sehemu iliyoathirika. Bila matibabu, mgonjwa anaweza kupata matatizo mengine ya kiafya au hata kufa.

Watu wengi hawawezi kusambaza maambukizi haya baada ya majuma mawili ya matibabu. Kwa hivyo, njia thabiti ya kumlinda mwenzio na hata nyinyi wenyewe ni kuhakikisha kwamba mhusika anafanyiwa uchunguzi unaofaa kubaini maradhi anayougua na kupata matibabu. Kumbuka kwamba kikohozi hiki chaweza kuwa ni kutokana na matatizo mengine kama vile maradhi ya pumu, mkamba (chronic bronchitis), ugonjwa wa kuvimba mapafu na kupumua kwa shida (emphysema), maradhi ya moyo au hata kansa.