Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Mbona hedhi nzito katika umri wangu?

March 17th, 2020 3 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Mimi ni mwanamke wa umri wa miaka 43. Katika kipindi cha miezi michache iliyopita nimekuwa nikishuhudia mzunguko usio wa kawaida wa hedhi zangu. Kwanza kabisa, hedhi zimekuwa zikitoka kwa wingi huku nikikumbwa na maumivu ya tumbo kana kwamba narejelea maisha yangu ya umri wa kubaleghe nilipoanza hedhi zangu. Mbona hivyo?

Lauryn, Nairobi

Mpendwa Lauryn,

Muda unavyozidi kusonga, mwili wa mwanamke huendelea kubadilika huku masuala mbali mbali yakichangia mabadiliko haya. Masuala haya ni pamoja na viwango vya homoni, kukatikiwa (menopause), ujauzito, matumizi ya mbinu za upangaji uzazi, mazingira, uzani, mazoezi miongoni mwa mambo mengine mengi. Masuala haya yanaweza kuathiri mzunguko wa hedhi kwa muda. Huenda ukashuhudia ishara kwa mara ya kwanza ukiwa na umri wa miaka 45, ilhali wengine huanza kushuhudia haya kutokea umri wa kubalehe. Hata hivyo, litakuwa jambo la busara kufanyiwa uchunguzi na mwanajinakolojia ambapo chunguzi kadhaa za kimatibabu zitafanywa ikiwa ni pamoja na pap smear na picha za fupanyonga (pelvic ultrasound) ili kuondoa shaka ya kuwepo kwa matatizo mengine kama vile fibroids, kuvimba kwa ukuta wa uterasi na kuvuja damu kupindukia.

 

Mpendwa Daktari,

Mimi ni mwanamume wa umri wa miaka 67. Nimekuwa nikikumbwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda. Mbali na tatizo hili, nimekuwa na uvimbe fulani mgongoni. Miaka kadhaa iliyopita, uvimbe sawa na huu uliondolewa, uchunguzi kufanywa na kubainika kwamba haukuwa na seli za kansa. Hata hivyo, uvimbe huu umerejea tena na una maumivu makali. Tatizo laweza kuwa lipi?

Humphrey, Mombasa

Mpendwa Humphrey,

Kuhusu uvimbe mgongoni mwako itakuwa vyema kupata ripoti kutoka kwa hospitali iliyokufanyia uchunguzi wa kwanza ili ujue aina ya uvimbe uliokuwepo hata kama haukuwa unasababisha kansa. Kisha sampuli itachukuliwa kutoka kwa uvimbe wa sasa kubaini ikiwa ni sawa na ule wa kwanza, au ikiwa umebadilika kwa njia yoyote. Kisha uamuzi huu waweza kufanywa kwa pamoja na daktari wako kuhusu mbinu mwafaka ya kukabiliana na uvimbe huu mpya.

Kwa upande mwingine, kisomo cha shinikizo la damu ni kipimo cha nguvu ambazo moyo wako hutumia kupiga damu, na uelekeo usio na nguvu dhidi ya mtiririko wa damu katika mishipa ya damu.

Shinikizo la kawaida la damu huwa kati ya 90/60mmhg na 140/90mmhg. Ikiwa ni juu ya 140/90mmhg linachukuliwa kuwa shinikizo la juu la damu.

Miongoni mwa kati ya asilimia 5 na 10 ya watu wanaokumbwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, tatizo hili husababishwa na jambo kama vile maradhi ya figo, matatizo ya kihomoni, ujauzito, anaemia, uvimbe, baadhi ya dawa. Kwa watu hawa, pindi tatizo hili likishatambuliwa na kukabiliwa basi shinikizo la damu litakabiliwa.

Miongoni mwa kati ya asilimia 90 na 95 ya walio na shinikizo la juu la damu, tatizo hili husababishwa na jambo fulani. Ni takwimu zinazoongezeka jinsi umri unavyozidi kuongezeka na ambapo shinikizo la damu likiwa juu, basi limekuwa likiongezeka pole pole kwa miaka nyingi.

Kuna baadhi ya mambo yanayohusishwa na shinikizo la juu la damu kama vile umri (kuwa zaidi ya umri wa miaka 40), kuwa mwanamume, kuwa wa asili ya Kiafrika, kuwa na jamaa wa karibu anayekumbwa na shinikizo la juu la damu, kuwa na kiwango cha juu cha chumvi, kiwango cha juu cha kalori, chakula kilicho na kiwango cha juu cha mafuta, kutofanya mazoezi, unene kupindukia, kunywa pombe kwa wingi, kuvuta sigara na msongo wa mawazo.

Habari mbaya ni kwamba mara nyingi hauwezi kujua kuwa shinikizo la damu liko juu hadi upimwe. Kwa hivyo, huenda ukahisi kama kawaida, ilhali shinikizo la damu linaendela kupanda na kuathiri mishipa ya damu. Hali hii yaweza kusababisha kiharusi, maradhi ya moyo, figo kukosa kufanya kazi na hata kupoteza uwezo wa kuona.

Ili kuzuia athari za kudumu, mgonjwa atapewa dawa za kupunguza shinikizo la damu na kurejea viwango vya kawaida. Ikiwa vipimo vya shinikizo la damu vitaimarika na kuwa vya kawaida basi dawa hizo zinafanya kazi. Ukisitisha matumizi ya dawa basi shinikizo la damu litarejea juu, na ndiposa ni muhimu sana kuendelea kutumia dawa ulizopewa.

Aidha, punguza kiwango cha chumvi unachokula, punguza kiwango cha mafuta na uwanga (starch) kwenye lishe yako, punguza unywaji pombe, koma kuvuta sigara, punguza uzani, fanya mazoezi, kula viwango vya juu vya mboga na matunda, pata usingizi wa kutosha na upunguze mawazo.