Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nimeona upele kifuani ingawa hauna maumivu

November 19th, 2019 2 min read

Na DKT FLO

KWA miezi kadha sasa nimekuwa nikikumbwa na upele usio na maumivu kifuani mwangu. Nini kinaweza kuwa kinasababisha shida hii?

Emily, Nairobi

Upele huu waweza kuwa unatokana na kung’atwa na wadudu, maambukizi ya ukuvu kwenye ngozi, maambukizi mengine ya virusi, mzio, eczema, chunusi, ngozi kugusana na kitu kinachosababisha mwasho, au maradhi yanayoathiri mwili wote kama vile lupus, maradhi ya kikoromeo (thyroid), ugonjwa wa ini. Itakuwa vyema ikiwa utafanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na daktari ili kichocheo kamili kitambulike na matibabu yanayofaa yaanze mara moja.

 

Nilishuhudia hedhi yangu ya kwanza nikiwa na umri wa miaka 14. Katika umri wangu wa kubalehe, nilikuwa nikikumbwa na maumivu makali ya tumbo miongoni mwa maradhi mengine. Hali iliimarika nikiwa katika miaka ya ishirini. Kwa sasa niko katika miaka ya thelathini na maumivu makali wakati wa hedhi yamerejea. Nini chaweza kuwa chasababisha hali hii na nitakabiliana vipi?

Mary, Mombasa

Maumivu makali wakati wa hedhi ni hali inayofahamika kama dysmenorrhea. Kuna aina mbili: primary na secondary. Primary dysmenorrhea hutokana na kunywea kwa ukuta wa uterasi wakati wa hedhi, na pia kuzalishwa kwa kemikali zinazofahamika kama prostaglandins na leukotrienes. Hali hii huanza miaka michache baada ya kuanza kushuhudia hedhi, na huathiri takriban asilimia 50 ya wanawake wote. Secondary dysmenorrhea husababishwa na matatizo ya kiafya kama vile fibroids, endometriosis au maradhi ya fupanyonga. Huanza baadaye maishani mwa mwanamke na tiba ya tatizo hili mara nyingi hukabiliana na maumivu. Yaonekana ulikumbwa na primary dysmenorrhea, hali ambayo imerejea lakini itakuwa vyema kuhakikisha kwamba hakuna tatizo linalochochea maumivu haya.Huenda severe dysmenorrhea ikahusishwa na hedhi inayotoka kwa wingi na kwa muda mrefu, awamu za kwanza za kukatikiwa, historia ya kifamilia ya kukumbwa na maumivu wakati wa hedhi, uvutaji sigara na uzani mzito. Tiba inahusisha dawa ya kudhibiti maumivu na kupunguza kunywea kwa uterasi. Hatua zingine ambazo huenda zikasaidia ni kufanya mazoezi, kujikanda tumbo kwa kutumia kitambaa kilichotumbukizwa kwenye maji yaliyopashwa moto na kupata usingizi wa kutosha. Ikiwa hali itazidi, tafuta ushauri wa mwanajinakolojia ili ufanyiwe chunguzi kadhaa.

 

Je kuna mbinu zingine za upangaji uzazi ambazo mwanamume anaweza kutumia ili kumzuia mkewe asishike mimba kando na kondomu?

Joel, Nakuru

Unaweza kuamua kutumia mbinu asili za upangaji uzazi kama vile kutoshiriki tendo la ndoa siku zisizo salama kwa mkeo. Hata hivyo mbinu hii itazaa matunda tu ikiwa mzunguko wa hedhi ya mkeo ni wa kawaida na mmefunzwa na mtaalamu wa mbinu asili za upangaji uzazi kuhusu jinsi ya kutambua siku ambazo hayuko salama. Pia mnaweza kutumia mbinu inayofahamika kwa Kiingereza kama withdrawal method, ambapo wakati wa tendo la ndoa unaondoa uume ukeni kabla ya kumwaga manii ili uyamwage kando. Mbinu ya kudumu ni vasectomy, ambapo mirija kwenye korodani inakatwa ili kuzuia manii yasitoke wakati wat endo la ndoa. Mbiu za kihomoni (tembe na sindano) kwa wanaume bado.