Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nina umri wa miaka 19 na sijaota ndevu, tatizo ni nini?

April 28th, 2020 2 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Mimi ni kijana wa miaka 19. Nilikamilisha shule ya upili mwaka jana lakini bado sijashuhudia ndevu hata moja usoni mwangu. Ni jambo la kuaibisha hasa ikizingatiwa kwamba wenzangu wamekuwa wakinyoa ndevu kwa miaka sasa. Je, nina tatizo na ikiwa ni hivyo, nifanyeje kurejea hali ya kawaida?

Msomaji

Mpendwa msomaji,

Ndevu ni mojawapo ya sifa za utambuzi kwa mwanamume. Sifa hii huanza kujitokeza katika umri wa kubalehe. Kuna baadhi ya wanaume ambao watajawa na ndevu wanapotimu umri wa miaka 18, ilhali kuna wengine ambao huenda wakasubiri hadi miaka ishirini au baadaye na hii ni kawaida. Kiamuzi kikubwa kinachobaini kasi cha ndevu kuota ni jeni. Hebu chunguza kutoka kwa jamaa zako wa karibu wa kiume kuhusu wakati walioota ndevu kwa mara ya kwanza. Katika umri wa miaka 40 mtu anaweza kuwa na ndevu zilizojaa ilhali zilianza kuota akiwa na miaka 34. Pili, ikiwa viwango vyako vya homoni za testosterone viko chini, basi huenda ndevu zako zikachelewa kuota au kasi ya kuota kwake ikawa chini. Hata hivyo ikiwa una viwango vya kawaida, basi vijalizo vya homoni hizi haviwezi kukusaidia.

Unaweza kaguliwa na mtaalamu wa ngozi kwa masuala kama vile matayarisho ya ngozi ambayo huenda yakachochea nywele hizi kuota. Kwa mfano kutumia krimu ya minoxidil, asilimia tatu peppermint oil au micro-needling. Pia, dumisha lishe bora, pata usingizi wa kutosha, subira na kufanya mazoezi.

Mpendwa Daktari,

Je, nitakabiliana vipi na vidonda vya mafua vinavyonitoka puani kila wakati?

Jared, Nairobi

Mpendwa Jared,

Vidonda vya mafua husababishwa na virusi vya Herpes Simplex. Watu wengi huambukizwa maradhi haya wakiwa utotoni na watoto wenzao, ambapo virusi hivi hujificha mwilini na kujitokeza unapokumbwa na msongo wa mawazo, ukiwa na mafua au mabadiliko ya kihomoni mwilini. Haiwezekani kukabiliana kikamilifu na vidonda hivi, lakini waweza kuvidhibiti kwa kutumia krimu za kupunguza uvimbe au dawa za kupunguza makali ya virusi hivi kwa ushauri wa daktari. Ukiwa na vidonda vya mdomoni, fukuta mchanganyiko wa maji yaliyopashwa moto na chumvi au dawa maalum ya mdomoni, jiepushe na vyakula au vinywaji moto; usile vyakula vilivyo na chumvi, viwango vya juu vya asidi au viungo vingi. Kunywa maji mengi na udumishe afya ya mdomoni.

Aidha, waweza nufaika kutokana na vijalizo vya virutubisho vya vitamini B na folic acid. Ikiwa vidonda hivi vitaendelea kwa zaidi ya wiki mbili pasipo kupona, basi unahitaji kufanyiwa uchunguzi na daktari.

Mpendwa Daktari,

Nina mimba ya miezi miwili na nimekuwa nikishuhudia madoa ya damu kwenye suruali zangu kwa siku tatu sasa. Je, hii ni kawaida, na ikiwa sivyo, nifanyeje kukabiliana na tatizo hili?

Karen, Mombasa

Mpendwa Karen,

Ni kawaida kushuhudia doa la damu wakati ambapo mimba inajitunga kwenye ukuta wa uterasi. Damu hii hutoka katika wiki za awali za ujauzito na mara nyingi huwa kidogo na huisha kivyake bila matibabu. Aidha, huenda ukavuja damu kutokana na mwasho kwenye lango la uzazi, maambukizi, mimba kujitunga nje ya uterasi (ectopic pregnancy) au hatari ya mimba kutoka. Litakuwa jambo la busara na la dharura kwako kumuona mwanajinakolojia ili ufanyiwe uchunguzi wa kimatibabu, ufanyiwe uchunguzi wa maabara na hata kupigwa picha za sehemu ya nyonga. Ikiwa mimba imejitunga nje ya uterasi na unavuja damu, upasuaji wa dharura hufanywa. Ikiwa kuna hatari ya mimba kutoka, huenda ukatibiwa na kurejea nyumbani, au ukalazwa hospitalini. Kuna wakati ambapo damu huanza kuvuja kuashiria kwamba tayari mimba imeanza kutoka, ambapo utapelekwa hospitalini na kutibiwa kwa kukamilisha shughuli hii.