Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nini kinachosababisha mwasho wa kila mara katika sehemu ya uke?

October 6th, 2020 2 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Ningependa kujua nini kinachosababisha mwasho wa kila mara katika sehemu ya uke?

Jane, Nairobi

Mpendwa Jane

Kwa kawaida aina nyingi za mwasho zinazokumba sehemu ya uke huwa za kawaida, lakini kutokana na sababu kuwa huenda hii ikawa ishara ya maradhi mengine, unapaswa kutafuta ushauri pindi unapoanza kushuhudia haya.

Hali hii husababishwa na mambo kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na:

•Bacterial vaginosis: Ni kawaida kuwa na mchanganyiko wa bakteria katika sehemu ya uke, lakini endapo bakteria hizi zitakuwa mbovu, basi hii yaweza pelekea maambukizi haya.

•Maradhi ya zinaa: ‘Chlamydia’, ‘genital herpes’, ‘genital warts’, ‘trichomoniasis’, na kisonono vyote husababisha mwasho katika sehemu hii.

•Maambukizi ya chachu (vaginal candidiasis): Hali hii hutokea kiwango cha juu cha chachu, kinapoota katika sehemu hii. Ujauzito, kushiriki tendo la ndoa, matumizi ya viua vijasumu, na kinga dhaifu mwilini vyaweza sababisha hali hii.

•Kukatikiwa: Kupungua kwa uzalishaji wa homoni ya estrogen mwilini kama inavyoshuhudiwa katika miaka ya kukatikiwa ya mwanamke husababisha kuta za uke kupungua na kukauka na hivyo kusababisha mwasho. Hali hii pia yaweza shuhudiwa miongoni mwa wanawake wanaonyonyesha.

•Kemikali: Kuna baadhi ya kemikali zinazopatikana kwenye baadhi ya krimu, kondomu na sabuni ambazo zaweza sababisha hali hii.

•Lichen sclerosis: Hii ni hali nadra ambayo husababisha madoa mepesi meupe kujiunda kwenye ngozi na hasa kwenye uke.

Ili kuzuia hali hii, usitumie visodo, karatasi za shashi, krimu, marashi na sabuni zenye harufu kali.

Tumia maji, sabuni isiyo na harufu kusafisha uke. Baada ya kwenda choo jipanguse kuanzia mbele ukirudi nyuma, valia suruali za ndani zilizoundwa kwa kitambaa cha pamba na uhakikishe unabadilisha suruali kila siku, badilisha nepi ya mtoto kila wakati, tumia kondomu unaposhiriki tendo la ndoa ili kuzuia maradhi ya zinaa na usijihusishe kamwe na ngono unaposhuhudia hali hii hadi utakapopata nafuu.

Ikiwa unashuhudia sehemu yako ya uke imekauka sana, tumia mafuta maalum ya kudumisha unyevu katika sehemu hii.

Usijikune kwani hii hueneza maambukizi.

Kwa kawaida hali hii huisha baada ya muda lakini unashauriwa kutafuta ushauri wa daktari kwa uchunguzi zaidi kubaini iwapo kuna tatizo kubwa.