PATA USHAURI WA DKT FLO: Tafadhali fafanua ‘siku salama’ katika masuala ya hedhi

PATA USHAURI WA DKT FLO: Tafadhali fafanua ‘siku salama’ katika masuala ya hedhi

Na DKT FLO

NILISOMA mawaidha yako kuhusu iwapo mwanamke anaweza kushika mimba iwapo atashiriki tendo la ndoa siku ya mwisho ya kushuhudia hedhi zake. Tafadhali eleza zaidi kuhusu jinsi ya kuhesabu siku salama kwa watu ambao hedhi zao sio za kawaida.

Grace, Kilifi

Mpendwa Grace,

Ni vigumu kuhesabu siku salama ikiwa hedhi zako sio za kawaida kwa sababu hauwezi kutabiri mzunguko utakavyokuwa mwezi ujao. Unaweza kuhesabu tu kurudi nyuma ili kukadiria siku ambayo huenda yai lililokomaa liliachiliwa kutoka kwenye ovari kwa kuhesabu siku 14 kutoka siku uliyopokea hedhi zako. Sababu nyingine inayofanya iwe vigumu kuhesabu siku salama ukiwa na hedhi zisizo za kawaida ni huenda unashuhudia haya kwa sababu mayai hayaachiliwi siku hizo. Hii inamaanisha kwamba yai huachiliwa mara chache kwa mwaka na hauwezi kujua haya kwa kuhesabu siku. Kuna baadhi ya watu wanaoshuhudia mabadiliko ya kimwili yai linapoachiliwa kama vile maumivu ya matiti, maumivu sehemu ya chini ya tumbo (upande mmoja), kutokwa na damu kidogo ukeni, ongezeko la ashiki na kutokwa na majimaji nzito ukeni kwa siku chache. Mbinu ya kipekee ya kuzuia mimba ikiwa hedhi zako sio za kawaida ni kwa kutumia vyema mbinu thabiti ya upangaji uzazi.

***

Nina rafiki ambaye ana virusi vya HIV lakini mkewe hana. Wote wanafahamu kuhusu hali zao na bado wanapendana. Wao hushiriki tendo la ndoa bila kinga na kwa miaka sasa mkewe hajawahi kuambukizwa virusi hivyo. Kuna uwezekano wa mke huyu kuambukizwa virusi hivi iwapo wataendelea kufanya hivi?

Jim, Nairobi

Mpendwa Jim,

Watu wa aina hii wanafahamika kama ‘discordant couple’ yaani, mmoja ana virusi vya HIV na mwingine hana. Kwa watu wa aina hii bila shaka kuna hatari ya maambukizi kila wanaposhiriki tendo la ndoa bila kinga. Hata hivyo, ikiwa yule ana virusi vya HIV anatumia dawa za kudhibiti makali ya virusi vya HIV (ARVs) na virusi vimedhibitiwa, basi uwezekano wa maambukizi ni finyu. Pia, yule asiye na virusi anaweza kutumia dawa za pre-exposure prophylaxis (PrEP) ambazo hutumiwa kuzuia maambukizi ya HIV kwa mtu ambaye kila mara yumo katika hatari ya kuambukizwa. Wahusika pia wanahitajika kujihepusha na mahusiano ya pembeni kwani yule asiye na virusi anaweza kuambukizwa kwingineko, na yule ambaye tayari ana virusi anaweza kuambukizwa upya na kupata aina tofauti ya virusi vya HIV.

 

Ni ishara zipi za mwanzo za maradhi ya kansa ya matiti na je mtu anawezaje kukagua matiti yake mwenyewe?

Jayne, Nairobi.

Mpendwa Jayne,

Ishara za kansa ya matiti ni pamoja na uvimbe kwenye titi, mabadiliko ya saizi na umbo la titi, kutokwa na maji maji yasiyo ya kawaida kwenye chuchu, ngozi kubadilika na chuchu kupinduka na kuangalia upande mwingine. Ishara hizi hujitokeza baada ya kansa kuenea kwa hivyo ni jambo la busara kujifanyia ukaguzi kila mwezi na kufanyiwa uchunguzi na mtaalamu wa kiafya kila mwaka.

Jifanyie uchunguzi kati ya siku tatu na tano baada ya hedhi. Anza kwa kuzikagua wakati mmoja kila mwezi. Kwanza simama mbele ya kioo kisha utazame matiti yote kuona iwapo kuna tofauti zozote za kimaumbo au ukubwa. Inua mikono yote juu ya kichwa chako na uone iwapo matiti yote yanasonga kwa usawa. Kisha lala chali alafu uweke mkono wako wa kulia chini ya kichwa chako. Ukitumia vidole vyako vitatu vya mkono wa kushoto finya titi lako kwa mwendo wa kulia ili uhisi jinsi titi lote lilivyo, kisha uchunguze chuchu. Kisha kaa chini uchunguze kwapa upande huo. Kisha finya kwa utaratibu chuchu kuona iwapo linatoa majimaji. Rudia utaratibu huu ukitumia mkono wa kulia kuchunguza titi na kwapa la kushoto. Ukifanya hivi kila mara, utajua jinsi matiti yako huwa, na hivyo utaweza kugundua mabadiliko yoyote ili uweze kumfahamisha daktari wako.

You can share this post!

MAZINGIRA NA SAYANSI: Mombasa hatarini kuzama baharini,...

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa pembeni ametimuliwa na mumewe,...

adminleo