Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Unene kwa wanaume unaathiri burudani?

November 26th, 2019 3 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Ni kweli kwamba kama mwanamume, unene unaathiri uwezo wako kitandani?

Kevin, Mombasa

Mpendwa Kevin,

Uzani mzito ni mojawapo ya hatari zinazosababisha matatizo ya kufanya tendo la ndoa kwa wanaume. Hii ni kwa sababu matatizo ya kihomoni, matatizo ya mishipa ya damu, mwili kuwa bwete na masuala ya kisaikolojia kama vile wasiwasi, mafadhaiko na kutojithamini. Uzani mzito aidha unahusishwa na matatizo kama vile kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya moyo, viwango vya juu vya cholesterol, matatizo ambayo huhusishwa na matatizo ya uwezo wa kushiriki tendo la ndoa vilivyo. Ili kukabiliana na tatizo hili dumisha lishe bora huku ukiongeza viwango vya mboga na matunda katika chakula chako, fanya mazoezi na udumishe uzani wenye afya. Pia, maradhi yanayohusika na hali hii kama vile kisukari na shinikizo la damu sharti yatibiwe.

 

Mpendwa Daktari,

Nina miaka 35 na bado sijapata mtoto. Hii ni kwa sababu nimekuwa nawashughulikia ndugu zangu, vile vile nimekuwa nikijaribu kuimarisha taaluma yangu. Nilikuwa nawazia kuanzisha familia pengine katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Nifanye hivyo au niwasikize wenzangu wanaonishawishi kufanya hivyo sasa ili nisichelewe?

Nelly, Nairobi

Mpendwa Nelly,

Mwanamke huzaliwa na mayai ya kumtosha. Idadi na ubora wa mayai hupungua umri unavyozidi kusonga. Wakati ambapo ni rahisi kushika mimba ni ukiwa chini ya miaka 30. Uwezo wa kushika mimba huanza kupungua ukitimu miaka 30 na hata zaidi ukishapita miaka 35. Ukifika miaka 40 yaweza kukuchukua miaka miwili ya kujaribu kabla ya kushika mimba. Kwa upande mwingine, uwezo wa wanaume kutungisha mimba huanza kupungua wakishatimu miaka 40, na pia umri wa mwanamume huathiri uwezekano wa mwanamke kushika mimba, iwe kwa njia ya kawaida au kupitia In vitro fertilization (IVF). Kutokana na sababu ubora wa mayai umeathirika, kupata mtoto baada ya miaka 40 huongeza hatari ya kukumbwa na matatizo. Pia, una uwezekano mkubwa wa kukumbwa na matatizo ya mji (placenta), kukumbwa na kisukari wakati wa ujauzito na pia kufanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua. Japo hatari hizi haziathiri kila mwanamke, ni wengi wanaokumbwa na matatizo haya. Mbali na hayo, masuala ya kijamii unayokumbana nayo hayaambatani na kinachoendelea mwilini mwako, na hivyo fanya maamuzi yanayokunufaisha.

 

Mpendwa Daktari,

Binti yangu atatimu miaka 17 mwaka ujao. Nahofia usalama wake kama msichana hasa katika enzi hizi za mtandao. Marafiki zangu tayari wamewasaidia watoto wao wasichana kuanza kutumia mbinu za upangaji uzazi na nilikuwa nafikiria pia mimi kufanya hivyo. Hilo ni jambo la busara?

Karen, Nairobi

Mpendwa Karen,

Baadhi ya wazazi hudhani kwamba kuwasaidia watoto wao kutumia mbinu za upangaji uzazi ni suluhisho la kujihusisha na masuala ya mapenzi kiholela. Lakini ukweli ni kwamba, hii inakabiliana na tokeo moja tu la kushiriki ngono; mimba zisizotarajiwa.

Hatari za kushiriki ngono kiholela ni pamoja na mimba zisizotarajiwa na uavyaji mimba, maradhi ya zinaa, virusi vya HIV, virusi vya Human Papilloma Virus (HPV) vinavyohusishwa na kansa ya lango la uzazi, matatizo ya mahusiano, dhuluma za kijinsia na kimapenzi, kutawaliwa kimawazo na matatizo ya kisaikolojia, miongoni mwa mambo mengine. Hatari hizi zitakuwepo maishani mwa binti yako kulingna na tabia yake, vile vile yeyote atakayekuwa naye katika uhusiano.

Habari mbaya ni kwamba hauwezi kumzuia dhidi ya haya yote. Mbinu bora ni kukuza uhusiano wa karibu wa kirafiki naye ili muweze kujadili kwa uwazi kuhusu tabia nzuri na mbaya.

Akihisi amekubaliwa na hahukumiwi atakufungukia na ataweza kukuambia kila anapohisi yuko katika mkondo hatari. Pia, jadiliana naye kuhusu kinachokubalika na usichokubali, na uwe tayari kusikia maoni yake.

Unapomtambulisha kwa mbinu za upangaji uzazi unawasilisha ujumbe kwamba hawajibiki na masuala ya uzazi. Utashangaa kujua kwamba yeye mwenyewe ana maadili yake na tayari ana mbinu ya kujilinda.

Kumbuka kwamba mbinu za upangaji uzazi pia zina athari zake akizitumia kwa muda mrefu.

Hata hivyo, ni wakati mzuri kuzungumza naye kuhusiana na masuala ya ngono.