Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: UTI husambazwa kupitia ngono?

October 22nd, 2019 2 min read

Na DKT FLO

MKE wangu amekuwa akikumbwa na maambukizi katika mfumo wa njia ya mkojo (Urinary Tract Infection – UTI) kila mara, na cha kushangaza ni kwamba amekuwa akinilaumu kwamba ni kutokana na udanganyifu wangu. Lazima nikiri kwamba nimekuwa na uhusiano wa pembeni na mwanamke mwingine lakini kila mara sisi hutumia kinga. Kwanza je, UTI husambazwa kupitia ngono? Na ikiwa sivyo, nini kinamsababishia mke wangu tatizo hili?

Kevo, Eldoret

Mpendwa Kevo,

UTI ni maambukizi ya mfumo wa kupitisha mkojo ambapo unajumuisha figo, ureter (mrija unaouganisha figo na kibofu) na kibofu. Kwa kawaida maambukizi ya UTI huwa yamekithiri miongoni mwa wanawake, na takriban asilimia 20 ya wanawake wote hukumbwa na maambukizi haya kila mara.

Baadhi ya watu wanaweza kupata maambukizi haya pasipo sababu, ilhali kwa wengine hutokana na muundo usio kawaida wa mfumo wa kupitisha mkojo, au kutokana na kisukari, mimba, matumizi ya dawa za kusisimua misuli, jeraha kwenye uti wa mgongo, matatizo ya neva, au matatizo mengine ya kingamwili.

Mara nyingi, bakteria zinazosababisha maambukizi haya huishi kwenye utumbo na zaweza kusafiri kutoka tupu ya nyuma hadi kwenye lango la mkojo kwani zinakaribiana. Kwa kawaida wanawake huwa na urethra (mrija wa mkojo kutoka kwenye kibofu) fupi wakilinganishwa na wanaume, suala linalorahisisha usafiri wa bakteria hadi kwenye kibofu na hivyo kusababisha maambukizi.

Bakteria hizi zaweza kuingia unapotumia choo kichafu kutokana na kurushiwa maji unapoenda haja, na pia kutokana na mgusano wa karibu wakati wa tendo la ndoa.

Maambukizi ya UTI hutibiwa kwa kutumia viua vijasumu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa mkojo. Ikiwa maambukizi haya yanajitokeza kila mara, anaweza kupewa kiwango kidogo cha viua vijasumu ambapo atahitajika kuvitumia kwa muda mrefu. Pia, huenda akashauriwa kutumia viua vijasumu kila baada ya kushiriki ngono au kutumia dawa hizi kwa muda mfupi (siku 1 au 2) kila anaposhuhudia ishara hizi.

Pia, anaweza kujifunza jinsi ya kufanya uchunguzi wa mkojo kila anaposhuhudia ishara. Kushiriki ngono na watu kadha huongeza hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa na pia husababisha kutoaminiana katika uhusiano.

Ili kuzuia maambukizi haya:

  • Aende msalani kila anapohitaji na ahakikishe kwamba anamaliza haja
  • Atumie choo kisafi kila mara
  • Anywe maji mengi kila siku na avalie suruali zisizombana
  • Avalie chupi zilizoundwa kwa kitambaa cha pamba
  • Ajipanguse kuanzia mbele kuelekea nyuma