Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Uvimbe ulitibiwa lakini umerudi tena

December 3rd, 2019 2 min read

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Babangu ana uvimbe mgongoni mwake. Ulichipuka miaka michache iliyopita ambapo ulikuwa mkubwa kiasi cha kwamba tulimpeleka hospitalini na akafanyiwa upasuaji kuuondoa. Mambo yalikuwa sawa hadi miezi mitatu iliyopita ambapo uvimbe huu ulianza kuchipuka tena. Tatizo laweza kuwa lipi na nini ambacho chaweza kufanywa kumrejeshea hali yake ya kawaida?

Robert, Mombasa

Mpendwa Robert,

Uvimbe mgongoni mwa babako waweza kuwa uotaji usio wa kawaida wa baadhi ya seli na tishu au kutokana na mkusanyiko wa usaha. Huenda uvimbe huo ukasababisha kansa. Njia ya kupekee ya kujua nini kinachosababisha uvimbe huu ni kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu. Utaratibu huu ungefanywa baada ya uvimbe wa kwanza kuondolewa. Ikiwa utaratibu huu ungefanywa basi sampuli ingechukuliwa kutoka kwa uvimbe huu. Pindi aina ya uvimbe huu ikitambulika basi daktari atakuambia ikiwa waweza kutibiwa au ikiwa kuna njia ya kuuzuia usichipuke tena.

 

Mpendwa Daktari,

Je, nitatofautisha vipi kati ya majimaji ya kawaida yanayotoka ukeni na yasiyo ya kawaida?

Vanessa, Nairobi

Mpendwa Vanessa,

Ni kawaida kwa wanawake wote baada ya kutimu umri wa kubaleghe kushuhudia majimaji katika sehemu ya ukeni. Kwa kawaida huu huwa mchanganyiko wa maji na seli ambazo husaidia kusafisha uke na kuhakikisha kwamba sehemu hii inasalia na unyevu, na hivyo kuzuia maambukizi. Majimaji hayo hubadilika kulingana na mzunguko wa hedhi. Pia hali hii yaweza kutokana na mazoezi, msongo wa mawazo au matumizi ya dawa za kihomoni. Rangi ya majimaji haya yaweza kuwa nyeupe au maang’avu. Yaweza kuwa nzito au nyepesi wakati tofauti wa mzunguko wa hedhi. Ni kawaida majimaji hayo kuwa ya hudhurungi au mekundu pindi kabla, wakati na baada ya hedhi.

Ikiwa majimaji haya ni ya rangi isiyo ya kawaida (manjano, kijani, wakati mwingine meupe) huku yakitoa harufu mbaya na kuwa mazito na kukusababishia mwasho basi inamaanisha kwamba una maambukizi. Maambukizi haya yanaweza kutokana na ukuvu, bakteria au viumbehai. Ili kujua nini kinachosababisha majimaji yasiyo ya kawaida na wakati mwingine kutofautisha baina ya majiamaji ya kawaida na yasiyo ya kawaida, sampuli yaweza kuchukuliwa na kufanyiwa uchunguzi. Ikiwa utapatikana kuwa na maambukizi yoyote basi utatibiwa. Wakati mwingine daktari ataitisha sampuli ya mkojo ili ufanyiwe uchunguzi.

 

Mpendwa Daktari,

Nini kinaweza kuwa kinasababisha upele katika sehemu inayozingira uke wangu?

Rose, Nairobi

Mpendwa Rose,

Upele katika sehemu inayozingira uke waweza kuwa kutokana na maambukizi ya ukuvu, bakteria au virusi. Pia yaweza kutokana na kuvimba na/au maambukizi katika vinyweleo vya vywele hasa baada ya kunyoa nywele za sehemu hii. Aidha, baadhi ya watu hupata upele huu kutokana na mabadiliko ya kihomoni kabla, wakati au baada ya kushuhudia hedhi. Pia, hii yaweza kutokana na matatizo ya ngozi yanayoathiiri sehemu zingine za mwili na hivyo kuenea hadi katika sehemu hii. Pia, yaweza kutokana na mzio. Ili kutambua kiini kamilli, unashauriwa kumuona daktari ili uchunguzi ufaao ufanywe na upate matibabu yafaayo.