Michezo

Patashika leo K’Ogalo wakiwashukia Bandari katika KPL

April 23rd, 2019 2 min read

Na CECIL ODONGO na CHRIS ADUNGO

SOFAPAKA wanaendelea kuselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya kuwakwaruza SoNy Sugar 1-0 wikendi iliyopita katika mechi iliyochezewa mjini Awendo.

Hata hivyo, huenda mabingwa hao wa 2009 wakapitwa leo na Gor Mahia wanaopigiwa upatu wa kuyazima makali ya Bandari FC ugani Moi, Kisumu.

Gor Mahia ambao ni wafalme mara 17 na mabingwa watetezi wa KPL, wamesakata jumla ya michuano 21. Wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 46 baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 na mabingwa mara nne Ulinzi Stars wikendi jana jijini Kisumu.

Nafuu zaidi kwa Gor Mahia ya kocha Hassan Oktay ni kwamba wangali na michuano minne zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo wapinzani wao wakuu Sofapaka wamezipiga hadi kufikia sasa.

Chini ya mkufunzi John Baraza, Sofapaka wanajivunia alama 48 baada ya kujibwaga uwanjani mara 25. Bao lao dhidi ya SoNy lilifumwa wavuni kwa njia ya penalti iliyochanjwa na mvamizi Umaru Kasumba.

Fowadi huyo mzawa wa Uganda anapigiwa upatu wa kumbwaga Allan Wanga wa Kakamega Homeboyz katika juhudi za kupigania taji la Mfungaji Bora wa KPL msimu huu. SoNy waliotawazwa wafalme wa KPL kwa mara ya mwisho mnamo 2006, wanajivunia jumla ya pointi 35.

Wakicheka dhidi ya Ulinzi Stars, Gor Mahia walichukua uongozi kunako dakika ya 47 kupitia kwa nyota wa zamani wa Harambee Stars Dennis ‘The Menace’ Oliech.

Ulinzi Stars inayonolewa kwa sasa na kocha veterani Benjamin Nyangweso hata hivyo ilisawazisha bao hilo katika kipindi cha pili kupitia penalti ya Enosh Ochieng aliyeangushwa na mlinzi wa K’Ogalo Geoffrey Ochieng ndani ya kijisanduku.

Licha ya sare hiyo, wanajeshi wa Ulinzi Stars bado wanashikilia nafasi yao ya nane kwa alama 33, mbili nyuma ya SoNy inayofunga mduara wa saba-bora.

Ushindi kwa Gor Mahia katika mchuano wa leo utawarejesha kileleni mwa jedwali na pia kuwapa hamasa ya kuipepeta Mount Kenya United kesho kutwa katika kipute kitakachowakutanisha uwanjani Kenyatta, Machakos.

Mabingwa wa 2008, Mathare United wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 39, mbili nyuma ya Kakamega Homeboyz ambao wanapania kuziba pengo la pointi nne linalotamalaki kwa sasa kati yao na Bandari wanaokamata nambari ya tatu baada ya kusakata mechi 23 chini ya kocha Bernard Mwalala.

Sare

Mathare wanaotiwa makali na kocha Francis Kimanzi, waliambulia sare ya 2-2 dhidi ya Vihiga United uwanjani Bukhungu, Kakamega mwishoni mwa wiki jana.

Chipukizi Lawrence Luvanda aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka kwa mabingwa mara 13 wa KPL AFC Leopards, aliiweka Vihiga United kifua mbele katika dakika ya saba. Dennis Wafula aliongeza bao la pili kunako dakika ya 67 baada ya kupokezwa krosi safi na Amos Kigadi.

Mshambulizi matata Cliff Nyakeya aliipa Mathare bao la kwanza kunako dakika ya 80 naye Johnstone Omurwa akatumia ulegevu kwenye safu ya ulinzi ya Vihiga kufunga bao la kusawazisha kunako dakika za mwisho wa mchuano huo.

Katika mechi nyingine, Posta Rangers ilijiondoa kwenye mduara hatari wa kushushwa ngazi kwa kuichapa Zoo Kericho 2-0 na kupaa hadi nafasi ya 15 ligini. Difenda wa Zoo Kericho Stanslaus Akiya alijifunga kabla Marcelus Ingotsi kufunga la pili na kuipa Rangers alama zote tatu muhimu. Matokeo hayo yaliwaacha Zoo FC ikiwa katika hatari ya kushushwa daraja.