Patrick Vieira apokezwa mikoba ya ukocha kambini mwa Crystal Palace

Patrick Vieira apokezwa mikoba ya ukocha kambini mwa Crystal Palace

Na MASHIRIKA

PATRICK Vieira, 45, ndiye kocha mpya wa Crystal Palace.

Kiungo wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, amepokezwa mikoba iliyoachwa na Roy Hodgson aliyeondoka mwishoni mwa msimu wa 2020-21 baada ya kuhudumu ugani Selhurst Park kwa kipindi cha miaka minne.

Vieira anakumbukwa zaidi kwa upekee na ukubwa wa mchango wake akiwa sogora wa Arsenal. Alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshindia klabu hiyo taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) bila kupoteza mechi yoyote mnamo 2003-04. Alisajiliwa na kocha Arsene Wenger mnamo 1997 na akaondoka kambini mwa Arsenal mnamo 2005.

Alisaidia kikosi hicho kunyanyua mataji matatu ya EPL.

Aliwahi pia kujezea Juventus, Inter Milan na Manchester City kabla ya kuangika rasmi daluga zake kwenye ulingo wa soka mnamo 2011.

Alianza ukocha akiwa katika akademia ya Man-City kabla ya kuhamia Amerika kudhibiti mikoba ya New York City inayoshiriki Major League Soccer (MLS) mnamo 2016.

Aliongoza kikosi hicho kukamata nafasi ya pili kwenye MLS kwa kipindi cha misimu miwili kabla ya kuhamia Nice mnamo 2018.

Katika misimu yake miwili ya kwanza kambini mwa Nice, aliongoza kikosi hicho kuambulia nafasi za saba na tano mtawalia. Alipigwa kalamu na Nice mnamo Disemba 2020 baada ya miezi 18.

Baada ya kuagana na Arsenal, Vieira ambaye alisaidia Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia mnamo 1998, aliwaongoza Inter Milan kutia kapuni mataji matatu ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kabla ya kuwanyanyulia Manchester City ubingwa wa Kombe la FA.

“Nina furaha kwamba Vieira amekubali mikoba ya kunoa kikosi cha Palace. Tuna mengi ya kufanya katika juhudi za kujisuka upya kwa msimu mpya. Vieira atashirikiana na Dougie kusajili wanasoka wapya watakaotusaidia kufikia malengo yetu,” akasema mwenyekiti wa Palace, Steve Parish.

Kibarua cha kwanza cha Vieira kambini mwa Palace ni kuongoza kikosi hicho kuvaana na mabingwa wa bara Ulaya, Chelsea katika gozi la EPL litalowakutanisha uwanjani Stamford Bridge mnamo Agosti 14, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Familia 50 zaumizwa na baridi kali baada ya nyumba zao...

AKILIMALI: Matumizi ya vitunguu kukabili kero ya wadudu...