PAUKWA: Bahati aonea soni kovu usoni pa mama

PAUKWA: Bahati aonea soni kovu usoni pa mama

NA ENOCK NYARIKI

SAA nne asubuhi, wazazi walianza kuingia shuleni kwa siku ya wazazi ambayo wanafunzi wa Tunu waliihamu sana.

Baadhi yao waliwasili kwa magari ya kifahari ambayo wanafunzi walikuwa na mazoea ya kuyaita mashangingi.

Wengine walikodisha teksi kutoka kwenye jiji la Rahaleo ili kuwasafirisha kuja kwenye shule hii ambayo iko kitalifa kirefu kutoka jijini.

Akina yakhe nao walishurutika kuuponda wa fisi ilimradi wajumuike na kufurahi pamoja na watoto wao katika siku hiyo muhimu ambayo iliandaliwa mwishoni mwa mwaka.

Bahati alikuwa ameketi darasani huku ameyatupa macho kwenye dirisha lililokuwa mkabala wa lango kuu. Aliona jinsi wanafunzi wenzake walivyokimbia mbio na kuwapiga pambaja wazazi wao.

Yeye aliendelea kuvuta subira. Alikuwa na hakika kwamba mmoja wa wazazi wake angehudhuria sherehe ile. Hata hivyo, aliomba kimoyomoyo asije! Jamani!….

Fikra zake zilipokuwa ziking’ang’ana na wazo fulani, mwanamke mwembamba mrefu alifungua lango la shule na kuingia ndani. Gauni refu la mavulia la rangi ya biti marembo alilolivaa lilimfanya kuonekana kimbaumbau mwiko wa pilau.

Shavu lake la kulia lilikuwa na kovu kubwa lililowanda mpaka sehemu ya pua na kuula kabisa mwanzi wa pua.

Moyo wa Bahati ulijiinamia kwa huzuni. Lile alilolihofia lilikuwa limejiri.

Kila wakati mama yake alipomtembelea shuleni, hakutaka wanafunzi na wazazi kufahamu kuwa alikuwa ndiye mama yake.

Kisa na maana! Lile kovu ambalo liliifanya sura ya mvyele wake kuchukiza…

HADITHI ITAENDELEA

You can share this post!

TALANTA: Dogo mtelezaji

MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu mkuu na mwandishi stadi

T L