PAUKWA: Bahati machozi tele kwa aibu ya mamaye

PAUKWA: Bahati machozi tele kwa aibu ya mamaye

NA ENOCK NYARIKI

MAMA yake Bahati alisimama kwenye uwanja wa shule huku amezubaa na kutunduwaa. Alitazama jinsi watoto wengine walivyowapokea wazazi wao kwa mlahaka.

Waliwapiga pambaja, wakawashika mikono na kuwaelekeza kwenye jukwaa la wageni ambapo walipokelewa na wanaskauti na kuonyeshwa mahali pa kuketi. Bahati hakuwepo kumkaribisha mama yake.

‘‘Kwa nini baba hakuhudhuria sherehe hii ilhali yuko nyumbani kwa likizo?” Bahati alijiuliza kwa sauti ya chini.

Ni kana kwamba kuja kwa mama yake kulitia kitumbua chake mchanga. Hakuona lolote la kufurahia na kuonea fahari jinsi walivyofanya wanafunzi wenzake.

Alijua fika kwamba baada ya maakuli, wenzake hao wangepita na kupituka kila mahali huku wakiwatambulisha wazazi wao kwa kila mmoja mle shuleni.

“Aisee! Mama yako yuko uwanjani anakuulizia,’’ Bahati alizinduliwa na sauti ya Dushi

Ili kujiondoa kimasomaso , aliinuka shingo upande kutoka dawatini pake na kufuatana na Dushi kuelekea uwanjani alikokuwa anasubiri Bi Cheusi.

Nje, baridi shadidi ilienea kote kote. Ndivyo huwa katika sehemu hii ya Rahaleo hasa mwezi wa saba ambao ndio mwanzo huwa umepisha msimu wa kipupwe.

Bi Cheusi alimtazama Bahati akimjia. Uso wa kijana yule daima ulikuwa mfano wa jalada la kitabu kwa mama yake. Haukuficha furaha ya kupindukia wala sononeko.

“Mwanangu leo una nini?” Bi Cheusi alimuuliza Bahati.

Uso ulimshuka Bahati na macho yakafungulia bilula za machozi.

HADITHI ITAENDELEA

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Wakulima wanaomba Nzoia Sugar iwalipe...

BI TAIFA JULAI 4, 2022

T L