PAUKWA: Biashara haramu ya Titi (sehemu 3)

PAUKWA: Biashara haramu ya Titi (sehemu 3)

CHUI mwingine aliyejificha kwenye matawi juu ya mti ambao Machugachuga alisimama chini yake alitishwa na mwangaza wa kurunzi.

Kufumba na kufumbua, alizichomoa kucha zake kali mithili ya misumari na akaruka kwa mori akatua juu ya dumu alilolibeba Machugachuga kichwani. Ghafla alilipiga lile dumu na kulipasua kwa kishindo paa! Mwangwi wa kishindo hicho ulijirudiarudia na kusikika hadi mbali.

“Uuui! Uuui! Uuuui! chui! Chui!” Machugachuga alipiga kamsa.

Kifo kilimkabili mkabala akavunja kiapo cha kutozungumza kwa sauti wakiwa msituni. Sasa hakuzungumza tu bali alipiga kamsa. Titi na mwenzake waliyabwaga chini madumu yao ya pombe haramu na kusema ‘mguu tuponye’. Walitimua mbio kimya kimya kurudi nyuma.

Machugachuga aliyekuwa amechanganyikiwa aliendelea kuchana mbuga kuelekea mbele huku akipigapiga kamsa. Sauti yake ilisikika hadi barabarani.

“Yuko wapi! Kimbia! Njoo tukusaidie!’’ sauti nyingine iliita kutoka hukoo barabarani.

Machugachuga alikimbia kuelekea kule ilikotokea sauti ile iliyoahidi msaada. Kumbe alikuwa amejigeuza ndege aliyejiongoza kwa hiari kwenye tundu la mwindaji. Alipofika barabarani, roho ilikuwa inamwenda mbiombio. Magoti si yake. Kiwiliwili si chake. Alimradi, alichoka kiwiliwili na akili.

Alipofika kwenye barabara ya lami, wingu kubwa lililofinga angani tayari lilikuwa limeanza kuachilia mvua. Ilianza kwa matone mazitomazito kisha rasharasha zilizoandamana na upepo mkali.

Rasharasha hizo zilianguka kwenye kichwa chake na kuyafanya macho kumwasha kutokana na pombe iliyommwagikia kichwani chui alipolipasua dumu. Sasa macho yaliingiwa na giza akakimbia kwa kuifuata sauti iliyomwita.

ITAENDELEA…

You can share this post!

TALANTA YANGU: Kiongozi wa maskauti

WANDERI KAMAU: Ukatili kwa wanahabari ni dalili za enzi za...

T L