Michezo

Paul Odera ndiye kocha mpya wa Kenya Simbas

May 31st, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limefagia benchi lote la kiufundi la timu ya taifa ya Kenya Simbas na kujaza nafasi hizo na maafisa wa timu ya Chipu wakiongozwa na Paul Odera.

Wembe uliowanyoa raia wa New Zealand Ian Snook (aliyekuwa kocha mkuu) na Murray Roulston (kocha) mwezi Januari, umewanyoa Wangila Simiyu (Meneja wa Timu), Christopher Makachia (Mtaalamu wa mazoezi ya viungo), Charles Ngovi (Naibu wa kocha), Dominique Habimana (Naibu wa kocha) na James Ondiege (Daktari wa timu), huku mtathmini wa timu Edwin Boit pekee akisalia.

Maafisa wanaoingia Simbas ni Odera (kocha mkuu), Jimmy Mnene (meneja wa timu), Ben Mahinda (mtaalamu wa mazoezi ya viungo), Boit (mtathmini wa timu), Michael Owino (kocha wa mazoezi ya viungo) na Albertus Van Buuren (kocha wa safu ya ulinzi).

Mwezi Aprili mwaka 2019, Odera aliongoza Chipu kurejea katika Raga ya Dunia ya daraja ya pili (JWRT) baada ya kuwa nje miaka 10. Chipu ilikanyaga Namibia 21-18 uwanjani Ruaraka na kujikatia tiketi ya kuwa nchini Brazil mwezi Julai 2019.

Amehitimu na kiwango cha tatu cha ukocha cha dunia na mkufunzi wa raga mwenye tajriba ya dunia.

Odera ni mwalimu wa masomo ya jiografia na sayansi katika Shule ya Upili ya Peponi House katika mtaa wa Kabete.

Mnene na Owino wamefanya kazi na Odera kwa miaka minne iliyopita katika benchi la kiufundi la Chipu.

Mahinda amekuwa akifanya kazi katika benchi la kiufundi la timu ya taifa ya wanawake almaarufu Lionesses.

Boit amefanya kazi na Chipu na Simbas katika majukumu yaliyopita akitathmini kila mchezaji na kutoa takwimu zao baada ya mazoezi na mechi.

Van Buuren alicheza katika shindano la Super Rugby mwaka 1996 kabla ya kuhamia New Zealand.

Lenana School

Amewahi kunoa Shule ya Upili ya Lenana.

Yeye ni Mkurugenzi wa Michezo katika Shule ya Kimataifa ya Crawford.

Odera ana ujuzi wa miaka 20 akifundisha shule nchini Kenya, Afrika Kusini na New Zealand.

Majukumu ya kwanza ya Odera kama kocha mkuu wa Simbas ni Kombe la Elgon dhidi ya Uganda mnamo Juni 22 mjini Kisumu na Julai 13 jijini Kampala.

Hakuna Kombe la Afrika (Gold Cup) mwaka 2019.

Shirikisho la KRU litaandaa mchujo wa kuunda timu ya taifa ya Simbas hapo Juni 1 uwanjani RFUEA jijini Nairobi.

Taarifa kutoka KRU zinasema kwamba Simbas itatafutiwa mechi zingine za kimataifa.

Aidha, KRU iko macho kufufua shindano la mataifa matatu la Victoria Cup kujaza nafasi iliyoachwa na kuondolewa kwa Gold Cup. Kombe la Victoria lilihusisha Kenya, Zimbabwe na Uganda.