Michezo

PAUL THIONG'O: Amewahi kutuzwa zawadi maalum na Zinedine Zidane

May 14th, 2020 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

AMEKUWA nchini Italia kwa kipindi cha miaka 11 na hivi sasa ana hamu sana ya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowakilisha Kenya katika mashindano na michezo ya kimataifa.

Katika kipindi hicho, Paul Thiong’o amekuwa Italia akipata mafunzo hadi kucheza soka ya kulipwa na anaamini anaweza kuchezea timu ya taifa ya Harambee Stars ingawa huko aliko anachezea timu ya Supa Ligi ya Rocchese Football.

Thiong’o alianza kuwa katika chuo cha mafunzo ya soka cha klabu ya Empoli FC kabla ya kuzichezea klabu za Colligiana, Lanciotto, Montelupp, Angri na sasa Rocchese.

“Nina hamu kubwa ya kukipiga katika timu ya taifa langu Kenya – Harambee Stars – kwani naamini nikipewa nafasi nitafanya vizuri. Nawaomba wale wahusika na uteuzi pamoja na afisi ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wanipe jaribio na ninaamini nitafuzu,” akasema kiungo huyo.

Ingawa mwanasoka huyu anachezea klabu ya Supa Ligi ya Italia, anaamini ana kiwango kikubwa cha kusakata soka na ana matumaini kama atafanyiwa majaribio ya kuichezea Stars, atawaridhisha wateuzi wa timu hiyo.

“Tuko Wakenya kadhaa tunaocheza klabu za madaraja ya chini lakini tuna viwango vikubwa vya kusakata kabumbu ya hali ya juu lakini tatizo kubwa ni kuwa wanaotambulika ni wale wanaocheza klabu zinazoshiriki katika Ligi Kuu pekee,” akasema.

Akiwa na umri wa miaka 24 sasa, Thiong’o amekuwa nchini Italia tangu alipokuwa kijana wa umri wa miaka 13, mwaka mmoja baada ya kuongoza kikosi cha timu ya Mombasa FC kilichoshiriki dimba la Danone Nations Cup mwaka 2007 mjini Lyon nchini Ufaransa.

Mwanasoka Paul Thiong’o (kulia) akiudhibiti mpira wakati akiwa na umri wa miaka ya utineja. Picha/ Hisani

Aliwavutia maskauti wa Empoli FC ya Italia iliyomfadhili kwa mafunzo ya soka pamoja na masomo.

Anasema anatamani Shirikisho la Soka Nchini Kenya (FKF) likishirikiana na serikali kuu pamoja na serikali za kaunti, kukusanhya na kuweka data za wachezaji wote Wakenya wanaosakata soka ng’ambo kwani kwa njia hiyo, wataweza kutambua wale wanaostahili kuchezea timu ya taifa.

“Sikuwa na bahati ya kiwango changu kutambulika nilipokuwa na umri wa miaka ambayo ningewakilisha taifa langu kwenye mashindano ya umri chini ya miaka 17, 20 na 23. Sasa nakumbusha kuwa tuko huku kwenye madaraja ya chini, FKF ifuatilie ijue hatua tunazopiga,” akasema.

Thiong’o ambaye ana hamu ya kupanda ngazi hadi kuchezea klabu ya Ligi Kuu ya Italia ya Serie A, amewahi kuibuka mchezaji bora katika mechi 11 kati ya mechi 18 timu yake imecheza.

Matukio hayo ya mchezaji bora yanaashiria kuwa ni mchezaji mwenye tajriba ya kusakata soka safi.

Mwanasoka Paul Thiong’o (kushoto). Picha/ Hisani

Wakati wa mashindano ya Danone Nations Cup, kiungo Thiong’o almaarufu ‘Zizzou’ aliibuka kuwa Mchezaji Bora na akatuzwa zawadi maalum na aliyekuwa mchezaji wa Ufaransa Zinedine Zidane ambaye kwa sasa ni kocha wa Real Madrid ya nchini Uhispania.

Anapoulizwa kuwa tangu aanze kukipiga huko Italia ni jambo gani alilotimiza maishani mwake na familia yake, Thiong’o anasema amemjengea nyumba mama yake mjini Kiambu.

“Nimeona umuhimu kwanza kumjengea nyumba mama yangu ndipo baadaye niangalie yale yangu ya binafsi,” akasema mwanasoka huyo.

Kwake, ametoa ombi kwa wachezaji wenzake Wakenya wanaocheza soka huko ng’ambo na hasa kwa timu za madaraja ya chini, wajitokeze kutambulika kwani huenda nao wakafuatiliwa maendeleo yao na kupata fursa ya kuchezea Harambee Stars.