Siasa

Pauline Njoroge ateuliwa mwangalizi wa uchaguzi Bangladesh

January 3rd, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

BLOGA Pauline Njoroge ameteuliwa kuwa miongoni mwa wataalamu kutoka Jumuiya ya Madola watakaohudumu kama waangalizi kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Bangladesh Jumatatu ijayo.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo, Bi Njoroge atakuwa miongoni mwa watu kumi kutoka mataifa tofauti duniani, ambayo ni wanachama wa Jumuiya ya Madola.

Watu hao wanatoka katika mataifa ya Jamaica, Cameroon, India, Kenya, Maldives, Nigeria, Papua New Guinea, Sri Lanka, Trinidad and Tobago na Uingereza.

Mwenyekiti wa ujumbe huo ni Waziri Mkuu wa zamani wa Jamaica, Bruce Golding.

Akirejelea uteuzi huo Jumatano, Bi Njoroge, ambaye pia ni Naibu Katibu wa Mipango katika Chama cha Jubilee (JP), aliutaja kuwa “hatua kubwa kwake mwaka unapoanza”.

“Huu ni uteuzi mkubwa katika safari yangu ya kisiasa. Ni matumaini yangu kuwa utanipa maarifa ambayo nitayatumia kuboresha hali ya kisiasa nchini,” alisema Bi Njoroge.

Kwemye mahojiano na ‘Taifa Leo’ hapo awali, Bi Njoroge alisema huenda akawania nafasi ya kisiasa ifikapo 2027.

“Mimi ni mkazi wa Nairobi. Hata hivyo, ninatoka katika Kaunti ya Kiambu. Bado sijajua nafasi nitakayowania, japo mipango hiyo ipo. Nitatoa maelezo zaidi baada ya kufanya uamuzi kamili kuhusu ni nafasi ipi na ni wapi nitakakowania,” akasema mwanablogu huyo.

Jumuiya ya madola inajumuisha nchi ambazo zilikuwa koloni za Uingereza.