Habari za Kitaifa

Pembejeo Feki: Upinzani waweka presha mawaziri Linturi, Miano wajiuzulu

March 24th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi amemtaka Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na mwenzake wa Biashara Rebecca Miano kujiuzulu kwa kufeli kuzuia uuzaji wa mbolea feki.

Amesema wasipofanya hivyo, ni wajibu wa Rais William Ruto kuwafuta kazi.

Kwenya taarifa, Bw Wandayi alidai mawaziri hao wanaruhusu vitendo vya kuhujumu uchumi kuendelezwa na asasi zilizoko chini ya usimamizi wao kupitia uuzaji wa mbolea na mbegu bandia.

“Inasikitisha kuwa wakati huu wakulima wamechanganyikiwa wasijue ni ipi mbolea halali na ni ipi feki,” akasema mbunge huyo wa Ugunja.

Pia alisema ni vigumu kutambua mbegu zilizoidhinishwa na zile bandia.

“Inakera kuwa katika msimu wa upanzi ndipo sekta hii imesheheni sakata moja baada ya nyingine kuhusu ubora, bei na uwepo wa pembejeo za kilimo,” akasema.

Waziri wa Kilimo anasimamia Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) na Shirika la Kukagua Afya ya Mimea (Kephis).

Naye mwenzake wa Biashara anasimamia Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs).

“Ni sharti wawajibikie hali hii kwa kujiuzulu,” akapendekeza Bw Wandayi.

Aidha, aliwataka maafisa wakuu wa Kebs na NCPB kujiuzulu ili kutoa nafasi kwa uchunguzi wa sakata hizo.

Bw Wandayi alimtaka Rais Ruto kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa mawaziri husika wanawajibikia sakata katika wizara zao.

Anataka serikali kuanzisha mpango mpya wa kununua, kuhifadhi na kusambaza mbolea na mbegu bora kwa manufaa ya wakulima.

Bw Wandayi pia anapendekeza kuwa wanajeshi (KDF) wakabidhiwe wajibu wa kusimamia ununuzi na usambazaji wa mbegu na mbolea ili kuzima ufisadi.

“Hii ni kwa sababu taasisi ambazo zimetwikwa wajibu huu zimefeli kabisa kuwakinga wakulima na Wakenya kutokana na magenge ya matapeli,” akaeleza.

Wito wa Bw Wandayi unajiri baada ya maafisa wa usalama kunasa mbolea feki katika kaunti za Kakamega, Baringo na Nakuru.

Aidha, shirika la Kebs liliwaambia wabunge kwamba kampuni ya SBL-Innovate Manufacturing Ltd imekuwa ikiuza mbolea feki kwa jina ‘GPC Plus Organic’ kupitia mabohari ya NCPB kote nchini tangu Januari 2023.

Kampuni hiyo imekuwa ikizua mbolea hiyo badala ya mbolea ya kiasili kwa jina, ‘BLC-GPC Original’ iliyoidhinishwa na Kebs mnamo Januari 28, 2023, na kupewa leseni yenye nambari ya ubora ya 60392.

“Mbolea hiyo feki ina kiwango cha juu cha pH na ni aina ya dolomite, yenye chembechembe za madini ya calcium, magnesium na carbonate ambazo hutumiwa kuboresha hali ya udongo. Lakini mbolea asili inayohitajika ni ile ambayo huongeza rutuba na kuchochea ukuaji haraka wa mimea,” Mkurugenzi Mkuu wa Kebs Esther Ngari akaambia Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo katika majengo ya bunge mnamo Alhamisi wiki jana.