Michezo

Penalti yasaidia Manchester United kutinga robo-fainali Europa League

August 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MANCHESTER United walihitaji bao la mwisho wa muda wa ziada kupitia penalti ya kiungo Bruno Fernandes ili kuwabandua FC Copenhagen ya Denmark kwenye robo-fainali za Europa League msimu huu.

Masogora hao wa kocha Ole Gunnar Solskjaer watakutana sasa na mshindi kati ya Sevilla na Wolves katika nusu-fainali. Itakuwa mara ya 17 kwa Man-United kunogesha kipute cha Europa League katika hatua hiyo ya nne-bora.

Licha ya kutokuwa katika ubora wao wa kawaida, Man-United walitamalaki mchuano wao dhidi ya Copenhagen na wakashuhudia teknolojia ya VAR ikiwanyima mkwaju wa penalti na kubatilisha bao walilolifungiwa na Marcus Rashford katika kipindi cha kwanza.

Kubisha kwingi kwa Man-United katika lango la Copenhagen hakukuwapa matunda waliyotarajia huku kipa Karl-Johan Jonhsson akipangua makombora aliyoelekezewa na Rashford nao Fernandes na Mason Greenwood wakishuhudia fataki zao zikibusu mhimili wa goli la wapinzani wao katika gozi hilo lililochezewa mjini Cologne, Ujerumani.

Ililazimu Man-United kutegemea ubunifu na utulivu wa Fernandes mwishoni mwa kipindi cha ziada ili kuweka hai matumaini ya kutia kapuni ufalme wa Europa League msimu huu. Penalti iliyopigwa na Fernandes ilikuwa ya 21 kwa Man-United kupokezwa hadi kufikia sasa msimu huu.

Johnsson alikuwa tegemeo kubwa la Copenhagen na alipangua jumla ya mikwaju 13 aliyoelekezewa na wavamizi wa Man-United. Copenhagen walikamilisha mechi bila ya jaribio lolote langoni pa Man-United.

Man-United walitawazwa mabingwa wa Europa League misimu minne iliyopita chini ya kocha Jose Mourinho ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Tottenham Hotspur nchini Uingereza.

Solskjaer anasalia sasa na michuano miwili pekee kabla ya kuwanyanyulia Man-United taji la kwanza tangu apokezwe rasmi mikoba ya kikosi hicho yapata siku 364 iliyopita.

Kurejea kwa Man-United kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao baada ya kuambulia nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ni zao la mchango mkubwa wa Fernandes.

Kiungo huyo mzawa wa Ureno alisajiliwa kutoka Sporting Lisbon kwa kima cha Sh9.5 bilioni mnamo Januari 2020. Ujio wa Fernandes umekuwa kiini cha ufufuo wa makali ya Man-United ambao kwa sasa wameanza pia kuhisi ukubwa wa mchango wa kiungo Paul Pogba kila anapowajibishwa na Mreno huyo kwenye safu ya kati.

Hadi Fernandes alipochezeshwa kwa mara ya kwanza kambini mwa Man-United katika mechi iliyowakutanisha na Wolves mnamo Februari 1, 2020, kikosi cha Solskjaer kilikuwa katika nafasi ya nane jedwalini huku pengo la alama 14 likitamalaki kati yao na Leicester waliokuwa ndani ya mduara wa tatu-bora.