Makala

Pendekezo gugumaji litumike kutengeneza mbolea, chakula cha mifugo

May 10th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa eneo karibu na Ziwa Kenyatta, Mpeketoni, Lamu sasa wanaunga juhudi za kufanya gugumaji liwe malighafi (raw material) badala ya kuendelea kuwasababishia kilio, ikiwemo kuchangia vifo vya samaki kila mara.

Gugumaji likiwa limememea katika sehemu mojawapo ya Ziwa Kenyatta, tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kila mara mmea wa gugumaji unapokua ziwani, huleta madhara, hasa iwapo mazingira unamokulia hutumiwa kwa shughuli mbalimbali za kila siku, ikiwemo uvuvi.

Gugumaji ni mmea wa rangi ya kijani kibichi ambao ukisheheni, hasa maziwani hugeuka kuwa kero kubwa.

Utapata mara nyingi wavuvi wakilalamika kupata mazingira magumu ya kuvua samaki kwenye maziwa yaliyoathiriwa na gugumaji.

Mmea huo pia unapomea ndani ya ziwa husababisha samaki kupungua kwani hukosa nafasi mwafaka ya kuzaana, ilhali hata wale wachache waliopo wakiishia kufariki kwa kukosa hewa safi ya kupumua.

Ni kutokana na hilo ambapo wasimamizi wa Ziwa Kenyatta, Kaunti ya Lamu, wavuvi na wakazi sasa wanaiomba serikali na wadau mbalimbali kujitokeza kubadilisha kilio chao cha kila mara kuhusu gugumaji  kuwa kicheko.

Wakazi hao wanapendekeza kuletwa wataalamu kwenye Ziwa Kenyatta watakaoibuka na mbinu za kuvuna gugumaji ziwani humo, kuliongeza ubora kwa kulitengeneza mbolea, chakula cha mifugo, mikeka na kadhalika.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Watumiaji wa Maji ya Ziwa Kenyatta (LAKWA), Bw Benson Kariuki, wakazi hao walisema hatua hiyo pia itasaidia kutunza hata zaidi mazingira ya ziwa hilo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Badala ya kuachwa kunyima wavuvi wetu kitega uchumi chao, ipo haja ya wataalamu kuletwa hapa kutuelimisha jinsi tutaweza kuvuna hili gugumaji na kulitumia kutengeneza bidhaa. Twafahamu kuna vile linaweza kutengenezwa mbolea. Wa kuunda vikapu, kadi, makaratasi na vitabu pia huunda kutokana na hili gugumaji,” akasema Bw Kariuki.

Mwenyekiti wa Miungano ya Wavuvi (BMU) Ziwa Kenyatta, Bw Samuel Musyoka, anashikilia kuwa njia rahisi ya kumaliza gugumaji ni kupitia mimea hiyo kufanyiwa uboreshaji na kutumika kutengenezewa vifaa mbadala vyenye manufaa kwa binadamu.

Bw Musyoka alilalamia kuwa kusheheni kwa gugumaji ziwani Kenyatta tayari kumechangia zaid ya aina tano ya samaki, hasa wale wa jadi kupotea kabisa miaka ya hivi punde.

Ziwa Kenyatta ndilo kubwa zaidi ambalo lina maji yasiyo ya chumvi kote Lamu.

 Linapatikana taarafa ya Mpeketoni, Lamu Magharibi.

Kulingana na Bw Musyoka, aina hizo tano muhimu za samaki zilizopungua zamani zilikuwa zikipatikana na kuvuliwa kwa wingi ziwani humo.

Aina ya samaki walioangamia kabisa kwenye Ziwa Kenyatta miaka ya sasa ni Mkunga, Ngorongoro, Mborode, Sire, Labeo (Nylon fish) na Mchokole.

Bw Samuel Musyoka, anasema walianza kuwakosa samaki hao kuanzia mwaka 2017 kwendelea.

Kati ya 2016 na 2017, Ziwa Kenyatta liligonga vichwa vya habari pale lilipokauka kutokana na kiangazi cha muda mrefu, hali iliyopelekea maelfu ya viumbe wa majini, ikiwemo samaki, vyura na viboko kufariki.

Hali hiyo pia ilisababisha wavuvi kukosa kazi kwani hawakuwa na mahali kwingine kwa kuendelezea uvuvi wao.

Miaka iliyofuatia baada ya 2017 hata hivyo ilishuhudia mvua, hivyo kupelekea Ziwa Kenyatta kujaa tena na kurejelea hadhi yake ya kawaida.

“Ziwa letu lilipokauka miaka ya awali na kisha kujaa tena maji, tumeshuhudia kukithiri kwa gugumaji kwa wingi miaka ya sasa. Linatatiza shughuli. Limechangia kupungua kwa samaki ilhali aina nyingine ikipotea kabisa ziwani hapa. Twaunga mkono waboreshaji bidhaa waje hapa kutufunza jinsi tutageuza hili gugumaji kuwa bidhaa za manufaa,” akasema Bw Musyoka.

Wavuvi wanasema ni aina tatu pekee za samaki wanaopatikana kwenye Ziwa Kenyatta lililojaa gugumaji.

Samaki hao ni Tilapia (Kiparapara), Mtonzi (Catfish) na Kamongo (Mudfish).

Kwa upande wake aidha, Afisa Mtaalamu wa Samaki kwenye Idara ya Uvuvi ya Kaunti ya Lamu, Bw Simon Komu, alisema changizo kuu inayopelekea samaki kupotea na gugumaji kukithiri Ziwani Kenyatta ni uharibifu unaoendelezwa na binadamu, ikiwemo ukulima na utumiaji wa mbolea ya sumu kando kando ya ziwa.

Bw Komu pia alitaja ufugaji, kuvua kupita kiasi na ukataji ovyo wa miti kando kando ya ziwa, hivyo kuchangia mabadiliko ya tabia nchi kwa ujumla.

“Sumu au kemikali inayofikishwa ziwani kufuatia mmomonyoko wa udongo kutoka mashamba ya wakulima imesheheni kwenye ziwa hilo. Kemikali imechangia ongezeko la rutuba ziwani, hivyo kutoa mazingira safi ya gugumaji kuendelea kumea na kunawiri,” akasema Bw Komu.

Awali, Ziwa Kenyatta lilijulikana kama Mkunguya lakini likabadilishwa jina na kubandikwa lile la Mwanzilishi wa taifa hili, Mzee Jomo Kenyatta miaka ya sabini (1970s).