Habari Mseto

Pendekezo kufadhili shule za kibinafsi lajadiliwa

August 6th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Chama cha Shule za Kibinafsi Nchini (KPSA) Mutheu Kasanga Jumanne alikuwa na wakati mgumu kuwashawishi wabunge kuunga mkono pendekezo lake kuhusu mpango wa ufadhili wa masomo ya shule za upili.

Chama hicho kinaitaka serikali kuzijumuisha shule za upili za kibinafsi katika mpango wake sasa wa kugharamia masomo sawa na inavyofanya katika shule za upili za umma.

Akiwasilisha ombi hilo jana mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu Bi Kasanga pia alipendekeza kuwa shule hizo zijumuishwe katika mpango wa serikali wa usambazaji vitabu shuleni.

“Mpango wa sasa ambapo wanafunzi wa shule za upili za kibinafsi hawaafidi kutokana na ufadhili wa Sh22,244 kila mwaka na vitabu vya kiada unakiuka kipengee cha 53 (1) cha Katiba. Kipengee hicho kinasema kuwa ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu yenye gharama nafuu na kwa usawa,” akasema Bi Kasanga.

Mwenyekiti huyo alisema sio haki kwa wanafunzi wanaojiunga na shule za upili za kibinafsi kutojumuishwa kwenye ufadhili wa serikali kama ilivyokuwa ikifanyika katika shule za msingi “ilhali data zao zimenakiliwa katika mfumo wa uhifadhi wa maelezo ya wanagunzi (NEMIS).”

“Hii ni kwa sababu kulingana na Sheria ya Elimu ya Msingi na mwongozo kuhusu utekelezaji wa Elimu bila Malipo serikali ilitenga bajeti ya Sh22,244 kwa kila mwanafunzi wa darasa la nane ambaye maelezo yake yalijumuishwa katika mfumo wa NEMIS kuhakikisha kuwa wote wanajiunga na shule za msingi,” Bi Kasanga akawaambia wanachama wa kamati hiyo walioongozwa na Mbunge wa Malava Malulu Injendi.

Aliwataka wabunge hao kuwasilisha pendekezo hilo la KPSA kwa wizara ya elimu ili wanafunzi hao wapate ufadhili wa serikali pamoja na vitabu vya kiada.

Hata hivyo, wabunge John Oyioka (Bonchari) na Theddeus Nzambia (Kilome)waliitaka KPSA kupunguza viwango vya karo vinavyotozwa katika shule za upili za kibinafsi kufidia ruzuku kutoka kwa serikali.

Bi Kasanga alikubaliana na pendekezo hilo lakini akafafanua kuwa kupunguzwa huko kwa karo kutalingana na fedha ambazo shule hizo zitapokea kutoka kwa serikali.

“Ndio tuko tayari kupunguza karo lakini kwa Sh22,244 pekee ikiwa serikali itakubalia na ombi letu,” akasema.