Habari MsetoSiasa

Pendekezo la Moses Kuria kuhusu sheria za uchaguzi

January 14th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria ametoa pendekezo tatanishi kuhusu namna ya kuendesha mazoezi ya uchaguzi nchini siku za usoni, akitaka viongozi wote wa kuchaguliwa  pamoja na viongozi wa vyama wawe wakitia saini mkataba kuwa watakubali matokeo ya uchaguzi jinsi yatakavyokuwa, hata iweje.

Bw Kuria, ambaye siku za majuzi amejipata kubanwa kutokana na matamshi yake, sasa anashauri timu iliyoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuendesha shughuli za kuunganisha taifa kuunda sera inayosema hivyo.

Kupitia akaunti yake ya Facebook Jumapili, mbunge huyo alisema kuwa viongozi wanafaa kukubali matokeo ya Urais, bila kujali yalipatikana kwa njia gani.

“Nina ushauri kwa timu inayounganisha taifa. Viongozi wote wa kuchaguliwa na viongozi wa vyama lazima watie saini mkataba kuwa watajukumika na kutii ‘mapenzi ya watu’ kwa kukubali matokeo ya uchaguzi bila kujali yanayofuata,” akasema Bw Kuria.

Matamshi yake Bw Kuria, hata hivyo, yanakuja wakati siasa za uchaguzi mkuu wa 2022 zimekuwa zikishika kasi, nacho chama cha Jubilee kudokeza kuwa Naibu Rais William Ruto hatakuwa mwaniaji Urais wa moja kwa moja, ila kutaandaliwa kura ya mchujo chamani.

Watumizi wa mtandao wa Fcebook hata hivyo, walikuwa na maoni mseto kuhusu pendekezo la mbunge huyo, japo wengine wakikashifu hali yake kuendeleza tabia ya kuchapa siasa za mapema.

“Jumbe zako hizi zenye maana fiche hazifai. Tumekuwa na uchaguzi uliogawanya taifa majuzi tu na uko hapa unaongea kuhusu uchaguzi mwingine. Haifai kabisa,” akasema Tony Smojo.