Habari MsetoSiasa

Pendekezo la Rotich kuhusu bodaboda lazidi kupingwa

June 18th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

BAADHI ya wabunge Jumatatu waliendelea kupinga pendekezo la Waziri wa Fedha Henry Rotich kuwa wahudumu wa bodaboda wawe wakigharamia bima za kuwalinda pamoja na wateja wao, wakilitaka bunge kulipinga litakapowasilishwa wakati wa kupitishwa kuwa sheria.

Waziri huyo akisoma bajeti alipendekeza wahudumu hao wawe na bima za kuwalinda, kulinda wateja wao, pamoja na watu wengine wanaoweza kuathirika wakipata ajali, kama mbinu ya serikali kukusanya ushuru zaidi, lakini viongozi mbali mbali wamekuwa wakipinga.

Wabunge Caleb Amisi (Saboti) na Antony Oluoch (Mathare) walisema mpango huo wa serikali utawazidishia mzigo wa kiuchumi wahudumu hao ambao uwezo wao ni wa chini na wakaapa kuwa watapinga pendekezo hilo wakati mswada wa fedha utawasilishwa bungeni kupitishwa.

Hata hivyo, walisisitiza kuwa hawapingi mipango ya serikali kuhusu mbinu za kukusanya ushuru, japo sehemu hiyo, ambayo itawalazimu wahudumu kugharamia bima zao wenyewe, za wateja wanaobeba na watu wengine wanaoweza kuathirika na shughuli zao.

“Hatukatai pendekezo hilo kikamilifu, tunazungumza kuhusu sehemu ambayo inapendekeza wahudumu wa Bodaboda wawe wakihitajika kuwa na bima ya kulinda kila kitu, kama mbinu ya serikali kutafuta pesa,” akasema Bw Amisi.

Wawili hao walikuwa wakizungumza bungeni wakati walifanya kikao na wanahabari.

“Pendekezo hili litakuja bungeni kama mswada wa fedha na litapitia utaratibu wa kawaida wa sheria bungeni. Tunawaomba wabunge wenzetu ambao walipigiwa kura kwa wingi na vijana walio katika sekta ya Bodaboda wasilipitishe jinsi lilivyo,” akasema mbunge huyo.

Bw Oluoch alisema Mkenya wa chini tayari amelimbikiziwa mzigo mkubwa wa kiuchumi na serikali, na hivyo kuongeza ushuru wa aina hiyo kutaharibu mambo, katika sekta ambayo inasaidia zaidi ya familia milioni tatu.

“Mbinu yoyote ya kukusanya ushuru sharti izingatie maslahi ya wananchi wa ngazi ya chini. Serikali haiwezi kutoza ushuru kwa kuwamaliza vijana wanyonge ambao walijitafutia kazi baada ya serikali yenyewe kushindwa kuwapa,” akasema Bw Oluoch.

Alisema mbinu hiyo ya kukusanya ishuru itavuruga sekta ya bodaboda na kuwasukuma wengi nje, hali ambayo itawakosesha wengi ajira na kuinua uwezekano wa kuongezeka kwa uhalifu.

“Serikali itafute mbinu mbadala katika suala hilo ambazo zitahakikisha kuwa wahudumu hawaathiriki. Sekta ya Bodaboda inasaidia zaidi ya watu milioni 10 nchini,” akasema.

Viongozi hao walizungumza baada yaw engine kutoa maoni sawa siku mbili zilizopita, wakihusisha Gavana wa Nairobi Mike Sonko na wabunge kadhaa.