Habari MsetoSiasa

Pendekezo la wabunge kuteuliwa mawaziri lapingwa

July 7th, 2019 1 min read

 Na Cecil Odongo

MUUNGANO wa Mashirika ya Kijamii umepinga vikali pendekezo la afisi ya bajeti ya Bunge la Kitaifa kutaka mawaziri wanaohudumu serikalini kuteuliwa kutoka kwa bunge ili kupunguza gharama ya matumizi ya serikali.

Kupitia taarifa, Mwenyekiti wa mashirika hayo, Bw Suba Churchill alikemea wabunge kwa kuwaeleza kwamba wamechangia ongezeko la matumizi hayo kutokana na idadi yao kubwa na pia kubobea katika ufisadi.

Bw Churchill pia alitoa wito kwa afisi hiyo kuwasilisha pendekezo hilo kwa Kamati ya Uwiiano(BBI) iliyobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta pamoja Kinara wa ODM Raila Odinga, ili Wakenya wafahamu uzuri au ubaya wake.

Vile vile alitaja pendekezo hilo kuwa njama ya kuunganisha asasi ya bunge na Mamlaka ya Urais ili kuzima uwajibikaji na mchakato wa kufuatilia serikali.

“Sababu kuu ya gharama ya juu ya matumizi ya serikali ni wabunge wenyewe ambao wana idadi kubwa. Kuteuliwa kwa mawaziri kutoka bungeni ni kuunganisha Urais na Bunge hali ambayo itazidisha ufisadi,” ikasema taarifa iliyotiwa saini na Bw Churchill.