Habari MsetoSiasa

Pendekezo rais ahudumu kwa miaka 4 na seneta miaka 7

May 17th, 2018 2 min read

Na LUCY KILALO

CHAGUZI za nyadhifa sita zinazofanywa nchini kwa wakati mmoja zinastahili kufanywa nyakati tofauti ili kupunguza joto la kisiasa kila baada ya miaka mitano, pamoja na kutoa nafasi kwa wanaoshindwa kuwania nafasi nyingine.

Mapendekezo hayo ya kubadilisha vipengee kadha vya Katiba, kulingana na mwasilishaji wake, yatahakikisha pia Wakenya wanawapiga msasa vilivyo wanaotaka uongozi.

Bw Ezekiel Njeru Namu aliambia Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Haki na Masuala ya Sheria kuwa kufanyika kwa chaguzi za urais, useneta, ugavana, ubunge na udiwani kwa wakati mmoja ndiyo chanzo cha vurumai zinazoshuhudiwa nchini kila baada ya miaka mitano.

Bw Njeru sasa anapendekeza mabadiliko, akimtaka rais na diwani kuhudumu kwa kipindi cha miaka minne na uchaguzi wao kufanyika pamoja. Naye gavana ahudumu kwa miaka mitano, mbunge kwa miaka sita na seneta kwa miaka saba. Hata hivyo, anataka nafasi ya Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ifutiliwe mbali.

“Nahisi tunastahili kubadilisha jinsi tiunavyofanya uchaguzi, kwani huwa tunaelekeza nguvu zote upande mmoja. Pia tutapunguza gharama ya uchaguzi,” alisema.

“Huwa tunakosa kuwahoji vilivyo wanaogombea kila mmoja binafsi. Wakenya hawajui tofauti ya viongozi hao kwani utapata watu zaidi ya 100 kila mmoja akiwania na akiwa na manifesto yake, na ndiyo sababu mwishowe tunapata viongozi ambao hatukutaka, kwa kuwa hatuna nafasi ya kuwapiga msasa vilivyo.”

Bw Njeru pia anasema kuwa uamuzi wake wa uchaguzi wa urais na diwani kufanyika wakati mmoja, ni kuhakikisha kuwa mwaniaji wa urais analazimika kufika mashinani, jambo ambalo kulingana naye halijakuwa likifanyika.

Pia anatetea jinsi alivyopanga vipindi vya kuhudumu, akisema kuwa vinapatia muda ikiwa ni maseneta, kukagua vilivyo utendaji kazi wa viongozi katika kaunti.

Aliambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Baringo Kaskazini, William Cheptumo kuwa nafasi kama ya Seneta ni muhimu na kwamba wanahudumia eneo kubwa, ambalo ni kaunti, na wanastahili kulipwa zaidi na sio kiwango sawa na wabunge.

Anataka pia suala la elimu lisizingatiwe kwa wanaowania nafasi hizo, pamoja na kuhimiza utumizi wa lugha ya mama katika bunge za kaunti.

Wakati huo huo, kamati hiyo pia ilisikiliza sababu za Bw Mohamed Mohamed Sheikh, ambaye anataka umri wa rais, usizidi miaka 70. Alisema kuwa majaji wanastaafu wakiwa na umri wa miaka 70, na watumishi wa umma miaka 60, hivyo rais na naibu wake wanastahili kuwa watumishi wa umma, na lazima umri huo wa kustaafu udhibitiwe.

Kamati hiyo itaangalia mapendekezo hayo na kuwapa wawasilishaji majibu katika kipindi cha siku 60 kuhusu uamuzi wao.