Habari Mseto

Pendekezo wanaochanga zaidi ya Sh100,000 waripoti kwa EACC

June 3rd, 2019 1 min read

Na SAMWEL OWINO

WATUMISHI wote wa umma wanaochanga zaidi ya Sh100,000 katika harambee watahitajika kutoa ripoti zao za ulipaji ushuru kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), ikiwa pendekezo jipya la sheria litapitishwa.

Kupitia kwa barua iliyoandikwa kwa Spika wa Bunge la Taifa Justin Muturi, Kiongozi wa Wachache Bungeni, Bw John Mbadi anataka sheria kuhusu maadili ya maafisa wa umma kufanyiwa marekebisho, ili maafisa wa umma wawe wakitoa ripoti hizo kwa EACC ndani ya siku 14 baada ya kuchanga, wakieleza mahali wametoa pesa hizo.

Mbunge huyo wa Suba Kaskazini amesema lengo la marekebisho hayo ni kukabiliana na ufisadi miongoni mwa maafisa wa umma, ambao wanapora pesa za umma na kuzitumia katika harambee.

Haya yamejiri wakati Naibu Rais William Ruto na wandani wake wanameendelea kujitetea dhidi ya maswali yanayoibuka kila kukicha kuhusu wanakotoa mamilioni ya pesa wanazochangisha makanisani karibu kila wikendi.

“Nataka maafisa wa umma wawe wakiishi kadri ya uwezo wao. Ikiwa michango yako huwa mamilioni katika hafla na haiolingani na mshahara wako, sharti ueleze EACC mahali umetoa pesa,” Bw Mbadi akasema.

Bw Mbadi pia anataka sheria ibadilishwe ili wananachi wawe wakifahamu utajiri wa maafisa wote wa umma.