Michezo

Pendekezo watumiaji wa pufya sasa watiwe ndani

July 31st, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limeahidi kuwaadhibu vikali na kukabiliana vilivyo na watimkaji wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwa lengo la kujitafutia ufanisi katika mashindano mbalimbali.

Katika mojawapo ya juhudi za kuyafikia haya, vinara wa AK wameefichua mpango wa kurai bunge kuwasilisha mswada utakaotoa mwongozo kuhusu ukubwa na ukali wa adhabu kwa wanaoshiriki uozo huu.

Kulingana na Peter Angwenyi ambaye ni Mwenyekiti wa AK katika eneo la Nyanza Kusini, wanariadha watakaopatikana na hatia ya kutumia pufya wanastahili kutiwa magerezani.

“Marufuku pekee haitoshi. Wanaoshiriki uovu huu wanastahili kupelekwa kortini, kushtakiwa na kuhukumiwa vifungo,” akasema katika kauli iliyowiana na ya Naibu Mwenyekiti wa AK, Paul Mutwii.

“Wanariadha walio na mazoea ya kutumia njia za mkato wajiandae kwa adhabu kali ya AK ambayo kwa sasa itashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Michezo na Kamati ya Maadili ya IAAF (AIU),” akaongeza.

Ilivyo kwa sasa, adhabu ambayo imekuwa ikitolewa ni ya mwanariadha aliyeshiriki matumizi ya pufya kuzuiwa kunogesha mashindano kwa muda fulani na hivyo kuweka nchi yake katika hatari ya kupigwa marufuku.

Zaidi ya kuharamisha matumizi ya pufya, vinara wa AK wanataka sheria ibuniwe ili kufanya kosa hili kuwa la jinai.

Makocha, mawakala wamulikwa

Kwa upande wake, Angwenyi anawataka pia makocha na mawakala watakaoshiriki uovu huu kupigwa marufuku ya kuhudumu humu nchini huku wanariadha wakinyimwa idhini ya kuwakilisha taifa katika mashindano yoyote mengine maishani.

Kenya kwa sasa inajiandaa kufanikisha mchujo wa kitaifa wa kuteua vikosi vitakavyowania nishani katika fani mbalimbali za Olimpiki za 2020 jijini Tokyo, Japan.

Kenya iliambulia pakavu katika Olimpiki za 1956 na 1960 ambapo ilishiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza.

Ilikuwa hadi 1964 ambapo ilitia kapuni nishani ya kwanza baada ya Wilson Kiprugut kujizolea medali ya fedha katika mbio za kita 800.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, karibu Wakenya 50 wamehusishwa na matumizi ya pufya, akiwemo mshindi wa zamani wa Boston na Chicago Marathon, Rita Jeptoo na Jemima Sumgong aliyeibuka malkia wa marathon katika Olimpiki za 2016 jijini Rio, Brazil.