Habari Mseto

Penzi la boi jirani tamu kuliko la mume wangu

February 21st, 2024 1 min read

Nimeolewa na nina watoto wawili. Hata hivyo nimependana na kijana jirani yetu mtaani. Ananipa penzi moto na nafikiria kumuacha mume wangu akikubali kuwa baba ya watoto wangu. Waonaje?

Kama umeamua kuvunja ndoa yako ili kufuata mapenzi, hiyo ni haki yako. Lakini pia zingatia tofauti ya umri kati yako na kijana huyo kwani anaweza kubadili nia baadaye.

Ex haachi nipumue na anajua nina familia

Miezi miwili iliyopita nilikutana na mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu. Tangu hapo amekuwa akinipigia simu akisema bado ananipenda. Nina familia na nilimwambia. Nifanyeje?

Nia ya mwanamke huyo ni kuvunja ndoa yako. Anataka muwe na uhusiano wa kando ili atumie nafasi hiyo kuharibu ndoa yako. Muepuke kabisa.

Amenigeuza shugadadi nigharimie maisha yake

Mpenzi wangu ana watoto wawili. Nimekuwa nikigharamia mahitaji yake na nataka kumuoa. Lakini kila nikimuuliza huniambia ningoje bila kunipa sababu au muda wa kungoja.

Hizo ni dalili kuwa mwanamke huyo hakupendi. Yuko nawe kwa sasa kwa sababu ya msaada unaompa. Ninaamini anaendelea kutafuta mpenzi wa dhati na akimpata atakuacha. Chukua hatua inayofaa.

Sitaki tuingie kwa ndoa na hana pesa wala kazi

Nilizaa na mwanamume aliyekuwa ameahidi kunioa. Alikuwa na kazi nzuri lakini baadaye alifutwa. Ananiambia bado anataka kunioa lakini najua hana uwezo wa kutunza familia.

Wajibu mkuu wa mwanamume katika ndoa ni kugharamia mahitaji ya familia yake. Hata kama ni mapenzi, utakosea kuolewa na mtu ambaye hana uwezo wa kukimu familia.