PENZI LA KIJANJA: Kuepuka uvundo wa upweke!

PENZI LA KIJANJA: Kuepuka uvundo wa upweke!

NA BENSON MATHEKA

LIZZ alifika kwa daktari wake akijihisi mgonjwa.

“Sifikirii vyema na kichwa kinaniwanga,” alieleza daktari.

Baada ya vipimo, hakupatikana na ugonjwa wowote japo hali hiyo ilikuwa imemsumbua kwa muda na ikabidi daktari kumhoji zaidi.

Katika mahojiano hayo, daktari aligundua kwamba Lizz alikuwa anasumbuliwa na upweke ulioathiri afya yake. “Upweke unaweza kuathiri afya yako ya kimwili na pia kiakili,” asema mwanasaikolojia James Kamangu wa shirika la Big Hearts.

“Wanasema upweke ni uvundo, nami ninasema upweke ni hatari. Unaweza kukusababishia madhara ya kiafya na kiakili. Kumbuka hata Mungu hakuumba binadamu mmoja. Aliumba wawili, tena na jinsia mbili. Hii inaonyesha umuhimu wa uhusiano wa kimapenzi katika maisha na afya za watu,” aeleza Kamangu.

Kulingana na Mwanasaikolojia Hara Marano, anayechangia katika jarida la Pyschology Today, kuna ushahidi kwamba mtu akikosa uhusiano wa kimapenzi na kwa kiasi kikubwa wa kijamii, afya yake ya akili na kimwili inadorora.

“Mahitaji ya mtu ya uhusiano wa kimapenzi na kijamii yanapokosa kutimizwa, uwezo wake wa kiakili na hata kimwili unasambaratika na matokeo huwa sio ya kufurahisha,” asema Marano.

Wanasaikolojia wanakubaliana kuwa athari za upweke hasa kwa mtu ambaye alikuwa katika uhusiano na akatendwa, huwa kwa akili na kwa mwili kwa wakati mmoja.

“Kwa baadhi ya watu, huwa wanakosa umakinifu, hamu ya kula na usingizi. Hii huathiri uwezo wao wa kufanya kazi na kutekeleza majukumu ya kimsingi katika maisha yao,” asema Kamangu.

Kulingana na mwanasaikolojia huyo, upweke unaweza kusababishia mtu shinikizo la damu, kuathiri uwezo wake wa kusoma na kukumbuka mambo.

Japo wanasaikolojia wanasema kwamba ni kawaida ya mtu kuhisi upweke nyakati tofauti za maisha yake, hali hiyo haifai kuruhusiwa kutawala kwa muda mrefu.

“Kuna tofauti ya hali ya upweke wa kawaida na upweke wa kukosa mapenzi au unaojiri pale mtu uliyezoea kuwa naye anapokuacha bila matumaini ya kumpata tena. Upweke wa kukosa mapenzi ni hali sugu na ukihisi umefikia kiwango hicho unapaswa kuona mtaalamu wa afya ya akili akushauri,” asema Kamangu.

Katika makala yake yenye kichwa Combating Loneliness, yaliyochapishwa katika Psychology Today, Marano anasema mtu akijipata katika upweke, kwanza anapaswa kukubali hali yake, kutafuta fursa ya kumwepusha na hali hiyo kama vile kushiriki katika makundi tofauti ya kijamii na kutafuta huduma za wataalamu.

“Epuka kuingia katika uhusiano kwa ajili ya kuponya hali yako bila uangalifu kwa sababu unaweza kujitumbukiza katika shida zaidi. Tafuta ushauri nasaha na ujipe muda kabla ya kuanza uhusiano mpya,” asema.

  • Tags

You can share this post!

FIFA yaidhinisha vikosi vya masogora 26 kwa ajili ya Kombe...

BAHARI YA MAPENZI: Kuboresha uhusiano baada ya ugomvi

T L