PENZI LA KIJANJA: Ndoa ni nipe nikupe, hakuna kuwa kupe tena!

PENZI LA KIJANJA: Ndoa ni nipe nikupe, hakuna kuwa kupe tena!

NA BENSON MATHEKA

UNATAKA kuolewa ili upate mume wa kukutunza uonekane na kuishi kama malkia?

Itabidi uwajibikie maisha yako dada kwa kuwa wanaume wa siku hizi hawataki kuoa vidosho wa kuwafyonza jasho lao tu.

Wanataka wasaidizi na sio watu wa kuwaongezea mzigo katika maisha yao. Kwa hakika, wanaume wengi siku hizi wanaambaa vipusa wakigundua hawataki kuwajibikia maisha yao wenyewe.

Wanasema hawataki kuoa yaya, kwamba wanaoa wake wa kusaidiana nao.

“Ndio, wanaume wa karne hii ni wa dijitali, hawataki kuona mtu wa kubadilika kuwa kupe. Wanasema wake wanaoketi kitako kutegemea waume zao ni analogi. Wanataka uje kwa maisha yao kuwa msaidizi, huo ndio ukweli wa maisha ya wakati huu na ndiyo mapenzi ya Mungu. Kwamba mume akioa huwa anapata msaidizi na sio mtumwa,” aeleza Bi Grace Wariara, wa kituo cha Abudant Love, Nairobi.

Hii ndio sababu wanaume wasiojua kupika, kuosha vyombo na kupiga deki kabla ya kuoa hawana bahati.

“Iwapo unataka kuoa msaidizi, itabidi nawe ujiwajibike pia. Lazima ujue kufua nguo kabla ya kuoa kaka, hauoi mashine ya kupiga dhobi na kisha utarajie mke arauke na kwenda kazini ili akusaidie kulipa bili zako,” asema.

Kwa hivyo mrembo, katika ndoa ya kisasa, kulaza damu ni hatia. Iwapo unatarajia mumeo kuwa ATM yako, utajuta, kumbuka kuwa uliolewa kuwa msaidizi, sio kupe.

“Unajua nini,” asema Wariara, “mwanadada anayeelewa kuwa ni msaidizi wa mumewe, hatabana pesa, atampeleka mumewe kujivinjari na kumnunulia zawadi. Hakuna sheria inayosema ni mwanamume pekee anayepaswa kudekeza mwanadada,” asema.

Mwanadada anayejua siri hii, huwa anamfanya mumewe kutoboka bila shida, na maisha yanakuwa shwari. Siri ni kufahamu kuwa katika ndoa, wewe ni msaidizi na sio kupe.

Na mume wa dijitali anaelezwa kuwa anaoa mke msaidizi na mpenzi na sio rafiki wa kike, kwa hivyo mwamini na pesa zako.

Wanawake wanajua kupanga mambo ya pesa sana, hasa pale wanapothibitisha kuwa wanathaminiwa.

“Kipusa naye anafaa kujiandaa kuwa mke, na kutema tabia za kuwa rafiki wa kike wa mtu kisha wafahamu kuwa uwezo wa kutunza boma iwe sawasawa, uko katika mikono yao, bila shaka kwa kusaidiana na waume zao kulea watoto, kufanya kazi na kupata pesa zao. Hivi ndivyo maisha ya kisasa ya ndoa yanavyohitaji na sio fikira na kasumba za zamani,” aeleza Dick Kasina wa shirika la Maisha Mema.

Msikize Kasina. “Ndoa ni ushirika, kujitolea, kuwajibika na kutunzana. Sio kitu cha bosi na mtumwa. Majukumu ni 50/50”.

  • Tags

You can share this post!

Wazazi hofu tele uteuzi wa shule ukianza

Raila aingia boksi ya Ruto

T L