PENZI LA KIJANJA: Raha ikizidi sana si raha tena!

PENZI LA KIJANJA: Raha ikizidi sana si raha tena!

NA BENSON MATHEKA

“MIMI nataka kufurahia maisha na hutanipimia hewa,” Daisy alimfokea mpenzi wake Tom.

Hii ilikuwa baada ya Tom kumshauri akome kulewa na kupenda raha sana ili wazingatie kujenga maisha yao ya baadaye. Daisy alipolipuka kwa hasira, akawa hasemezeki, Tom alimuacha

“Niligundua kwamba Daisy hakutofautisha furaha na anasa. Nilikuwa nimejitolea kumpa maisha ya furaha kadiri ya uwezo wangu lakini akachagua anasa,” asema.

Ni kauli ambayo wataalamu wa masuala ya mahusiano wanakubaliana nayo wakisema kwamba watu wengi wanaharibu maisha ya mapenzi kwa kupenda anasa.

“Mtu anafaa kutofautisha au kuchunga asitumbukie katika anasa na kuzama akidhani anasaka raha. Raha bila mipaka ni anasa na huwa hatari sana. Kuna watu wanaozoea anasa hadi wanashindwa kujidhibiti na sasa wanajuta,” asema Ashley Kimani, mtaalamu wa masuala ya mahusiano wa shirika la Love Care Nairobi.

Anasema japo watu wanahitaji raha katika maisha, baadhi hawajui kuipima.

“Mtu akishindwa kudhibiti raha inaweza kuwa kizingiti kwa maisha yake ya mapenzi. Inasemwa kuwa raha haina mwisho na huo ndio ukweli wa mambo. Baadhi ya watu huwa wanaponda raha hadi wanasahau mambo muhimu kama kuweka msingi imara wa maisha yao. Anasa inavuruga mustakabali wa maisha ya mtu,” asema Ashley.

Kulingana na Pesha Asman, mwanasaikolojia katika kituo cha Rai Mufti, Nairobi, anasa ni kupenda raha kupita kiasi.

“Watu wana njia tofauti za kujipa raha. Lakini ikiwa huwezi kudhibiti utashi wako wa raha, basi inabadilika na kuwa anasa ambayo ni hatari kwa maisha hasa ya ndoa,” asema Pesha.

Mwanasaikolojia huyu anasema kizazi cha sasa kinashindwa kudumu katika ndoa kwa sababu hakiwezi kutulia kikifuata anasa.

“Imekuwa vigumu kwa kizazi cha sasa kudumu katika ndoa kwa sababu inawafunga. Kinataka maisha ya ‘free style’ ili kiweze kufanya kinavyotaka. Badala ya kutafuta maisha ya furaha kinakamia maisha ya anasa; kulewa, kutalii, kucheza densi, kula ufuska na kulala,” asema Pesha.

Wataalamu wanasema kwamba watu wengi wamepotoka wakidhani raha ya maisha ni kuburudika vilabuni na ufuska.

“Kuna shughuli zinazoweza kupatia mtu raha huku akidumisha heshima ya taasisi ya ndoa. Raha kama hii inaweza kupeanwa na watu wawili wanaopendana na kuridhishana,” asema Ashley.

Pesha anaongeza kuwa ukosefu wa maadili umechangia hali ya sasa ya kupenda anasa.

“Unapata mwanadada anapatia kipaumbele shughuli zake za burudani badala ya mumewe naye mume anachangamkia kivyake pembeni kuliko kuwa na mkewe,” asema.

You can share this post!

Uaminifu wa Mutua kwa Ruto wayumba

Tottenham wapepeta Southampton 4-1 katika EPL

T L