PENZI LA KIJANJA: Ukitaka kumjua ‘gold digger’, bana mikoba

PENZI LA KIJANJA: Ukitaka kumjua ‘gold digger’, bana mikoba

NA BENSON MATHEKA

KWA wiki sita, Jonas alikuwa akijaribu kumpigia simu Lily bila mafanikio.

Alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanadada huyo kwa mwaka mmoja na hii ilikuwa tabia yake.

Juzi, Lily alimpigia simu na baada ya salamu, alitoa ombi ambalo Jonas alikuwa amezoea.

“Alinitaka nimtumie Sh100,000 akisema alikuwa na dharura,” asema barobaro huyo ambaye ni meneja wa huduma za wateja katika benki moja jijini.

Kitu ambacho Jonas alikuwa na hakika nacho na kilimfanya kutafuta ushauri ni kuwa Lily angekatiza mawasiliano hadi wakati atakapotaka pesa kutoka kwake au kupelekwa kujivinjari Dubai au Afrika Kusini.

“Ukijipata katika hali kama hii, jua unachezwa. Mtu ambaye hadumishi mawasiliano hakupendi, ikiwa haja yake ni pesa kutoka kwako huyo ni gold digger, anakutumia tu. Hana haja na wewe, anamezea mate pesa zako,” asema mwanasaikolojia George Kimani wa shirika la Love Care Nairobi.

Kimani asema kuna watu ambao wamebobea katika kuchezea shere wengine wakijifanya wapenzi.

“Kuna watu ambao kazi yao ni kunyemelea walio na pesa na kujifanya wapenzi ilhali lengo lao ni kuwafyonza pesa. Kuna wanaume na wanawake ambao wamebobea katika hulka hii. Baadhi wanaifanya kama kazi rasmi,” asema Kimani.

Rosalie Wanjiru, mtaalamu na mtafiti wa masuala ya mahusiano ya mapenzi, anasema kwamba watu wengi wamefadhaika baada ya kuangukia gold diggers wakidhani ni wapenzi wa dhati.

“Kuna watu ambao wamepoteza mamilioni na kufilisika wakijaribu kufurahisha vipusa na barobaro wanaowania pesa zao. Baadhi wameishia hospitalini,” asema.

Wataalamu wanasema kwamba wenye tabia hii huwa wanabadilisha mbinu kulingana na windo wanaloangukia.

“Huwa wanapima mtu kwanza ili kujua chanzo cha mapato yake kisha wanamweka boksi na kuanza kumfyonza. Inahitaji busara ya juu kugundua mapema kabla ya kutumbukizwa kwenye shimo la kina kirefu na mapenzi ya aina hii,” asema Wanjiru.

“Maneno yao wakitaka utoboke hela au uwapeleke likizo au kujivinjari huwa ya kumtoa nyoka pangoni. Wakipata wanachotaka kwako wanaingia mitini hadi watakapojitokeza na hitaji lingine la pesa,” asema Wanjiru.

Kimani asema kwamba japo awali ni vipusa waliokuwa na tabia hii, siku hizi barobaro pia wamekuwa mabingwa wa kufyoza vipusa.

“Barobaro wamebobea katika hulka hii ambayo awali ilihusishwa na vipusa. Wanawanyemelea vipusa wenye mishahara mikubwa, wanaotoka familia za mabwenyenye na wanawake walio na mali,” asema.

Wanjiru asema watu waliobobea katika tabia hii huwa wanaacha mtu kwa mataa wakigundua mapato yake yamepungua au akibana mikoba yake.

“Ukitaka kujua iwapo mtu anakupenda kwa dhati, bana mikoba. Lugha itabadilika ukose kuitwa yale majina matamu uliyokuwa ukisikia ulipokuwa ukimpa hela,” asema.

You can share this post!

Cologne yazamisha chombo cha Borussia Dortmund katika...

UJAUZITO NA UZAZI: Tatizo la kuendelea kuvuja damu baada ya...

T L