Habari

PENZI LA MAUTI: Mume na mpango wa kando wazuiliwa kwa mauaji ya mkewe

January 30th, 2019 2 min read

Na ERIC WAINAINA

MWANAMUME alifikishwa katika mahakama ya Kiambu Jumanne pamoja na mwanamke anayeshukiwa kuwa mpenzi wake wa kando kwa madai ya kumuua mkewe.

Hakimu Stella Atambo aliwakubalia polisi kuzuilia wawili hao, Joseph Kori Karue na Judy Wambui Mungai katika rumande kwa siku 14, ili kuwapa muda wa kukamilisha uchunguzi kuhusiana na mauaji ya Mary Kamangara mnamo Jumamosi iliyopita.

Wawili hao, ambao upelelezi unaelekeza uwezekano wa kuwa kwenye mapenzi ya kando, walikamatwa kwa madai ya kushirikiana kumuua Mary nyumbani kwa Judy katika mtaa wa kifahari wa Four Ways Junction, kwenye barabara ya Kiambu.

Kulingana na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wanaochunguza mauaji hayo, Mary, ambaye alikuwa na umri wa miaka 39, alidanganywa na Judy wakaenda nyumbani kwake, ambako bila ufahamu wake mumewe alikuwa anasubiri, ndipo akakumbana na mauti yake.

Polisi walieleza Taifa Leo kuwa kabla ya kwenda Four Ways Junction, Judy na Mary walizuru klabu ya Homeland kwenye barabara ya Thika, ambako walikula nyama choma na hata wakapigwa picha wakiwa pamoja.

Judy, ambaye wapelelezi wanakisia kuwa na umri wa chini ya miaka 30, ndiye aliyemwalika Mary waende Homeland. Marehemu alikuwa akifanya biashara ya kuuza bidhaa za ujenzi mtaani Kahawa West.

Wapelelezi walidokezea Taifa Leo kuwa mapema siku hiyo, Judy alikodisha gari ambalo alitumia kwenda kwa nyumbani kwa Mary mtaani Safari Park Gardens, ambako walikaa kwa muda kisha wakaenda Homeland kula nyama choma.

Kisha walienda nyumbani kwa Judy mtaani Four Ways Junction wakitumia gari aina ya Mercedes Benz lake marehemu. Gari la lililokuwa limekodishwa na Judy awali liliachwa Homeland.

Kulingana na polisi, walipofika nyumbani kwa Judy, Mary alishtuka kumpata mumewe Kori humo, na ni hapo ambapo purukushani ilizuka na Kori akamgonga Mary kichwani kwa bastola yake aina ya Ceska, na akaaga dunia papo hapo.

Judy na Kori wanaripotiwa kupanga njama ya jinsi wangetupa mwili wa Mary, na mpango wao wa kwanza ulikuwa wa kuomba huduma za teksi. Lakini dereva alikataa kazi hiyo alipofahamu ilikuwa ya aina gani. Polisi wanamtafuta dereva huyo ili awape habari zaidi.

Baada ya mpango huo kutibuka, wawili hao waliamua kubeba mwili wa marehemu kwenye gari lake, ambapo wanadaiwa waliupeleka hadi bwawa la Courtsey Beach karibu na Ruiru, mahali ambako ulipatikana Jumapili kando ya bwawa.

Wapelelezi wanaochunguza mauaji hayo walisema wanatafuta picha za CCTV kutoka hoteli ya Homeland na pia za mtaa wa Four Ways Junction ili kufahamu yaliyotokea, na pia jinsi mwili wa marehemu ulivyosafirishwa kutoka hapo hadi bwawa la Courtsey Beach.

“Bado hatujapata picha za CCTV za Homeland na mtaa wa Four Ways Junction ambako uchunguzi wa mapema umeonyesha marehemu na mshtakiwa wa pili (Judy) walionekana,” Inspekta Cornelius Arwasa aliambia mahakama katika taarifa.

Katika nyumba ya Judy, polisi kutoka kituo cha Juja, ambao ndio wanaochungua mauaji hayo, walipata nguo zilizokuwa na matone ya damu, ambayo walisema yatasaidia kupata DNA muhimu kwenye uchunguzi wao.

Kulingana na majirani, Kori alikuwa akitembea nyumbani kwa Judy mara kwa mara hasa usiku ambako alikuwa akitoka asubuhi.

“Huyo jamaa anajulikana hapa kwa sababu hutembea nyumbani kwa Judy mara nyingi. Tukiona ameegesha gari lake la Toyota Lexus hapa huwa tunajua yuko huku,” jirani mmoja aliambia Taifa Leo.

Polisi wangali wanatafuta liliko gari la marehemu huku marafiki wakimtaja Kori kama “jamaa mtulivu”.