Michezo

Pep alenga UEFA

July 27th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO 

KOCHA Pep Guardiola amesema Manchester City watapata hamasa ya kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya kuridhika kutokana na mafanikio ya kufuzu kipute hicho muhula ujao wala si kwa kubatilishwa kwa marufuku ya Uefa.

Mnamo Februari mwaka huu, Bodi ya Uefa inayodhibiti matumizi ya fedha miongoni mwa klabu za bara Ulaya (CFCB) iliwaadhibu Man-City kwa kukiuka kanuni za matumizi ya fedha (FFP) kati ya 2012 na 2016. Adhabu hiyo ilikuwa ni marufuku ya kutoshiriki kivumbi cha UEFA kwa misimu miwili na faini ya Sh3.5 bilioni.

Ingawa hivyo, mahakama ya kimataifa ya mizozo ya spoti (CAS) ilibatilisha maamuzi hayo ya awali ya Uefa mnamo Julai 13 na kupunguza faini ambayo Man-City walitozwa jadi Sh1.2 bilioni pekee kwa hatia ya kutatiza uchunguzi dhidi yao walipokosa kushirikiana vilivyo na vinara wa Uefa.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Real Madrid katika marudiano ya hatua ya 16-bora mnamo Agosti 7 ugani Etihad huku wakijivunia ushindi wa 2-1 kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza.

Ushindi au sare dhidi ya Real katika gozi hilo itawapa Man-City tiketi ya robo-fainali dhidi ya mshindi kati ya Olympique Lyon na Juventus.

Man-City hawajawahi kusonga mbele zaidi ya hatua ya nusu-fainali kwenye kivumbi cha UEFA ambacho kocha Guardiola alikinyanyua mwisho akidhibiti mikoba ya Barcelona mnamo 2011.

Mapambano yote ya robo-fainali, nusu-fainali na fainali ya UEFA yatachezewa jijini Lisbon, Ureno kati ya Agosti 12-23. Mechi za robo-fainali zitaanza kupigwa Agosti 12 katika uwanja wa Jose Alvalade. Nusu-fainali zitaandaliwa kati ya Agosti 18-19 uwanjani Sport Lisboa Benfica kabla ya uga huo kuwa mwenyeji wa fainali mnamo Agosti 23.

Mshindi wa hatua ya 16-bora kati ya Bayern Munich na Chelsea watakutana na mshindi kati ya Barcelona na Napoli katika hatua ya robo-fainali. Ingawa hivyo, Chelsea wana nafasi finyu ya kupita mtihani mgumu wa Bayern mnamo Agosti 8 uwanjani Allianz Arena.

Chini ya kocha Frank Lampard, Chelsea watashuka dimbani wakilenga kubatilisha kichapo cha 3-0 walichopokezwa na Bayern katika mkondo wa kwanza uwanjani Stamford Bridge.

Chelsea na Man-City watakutana katika nusu-fainali iwapo watafaulu kuwabwaga wapinzani wao kwenye hatua ya nane-bora.

Bayern na Man-City ambao wanawania ufalme wa UEFA kwa mara ya kwanza katika historia, ndio wanaopigiwa upatu wa kutia kapuni taji la kipute hicho msimu huu.

“Sioni kikubwa kitakachotuzuia kunyanyua ubingwa wa UEFA msimu huu iwapo tutawaangusha kirahisi Real Madrid ambao ni wafalme wa shindano hilo,” akasema Guardiola kwa kukiri kwamba atakuwa amefeli pakubwa iwapo atabanduka uwanjani Etihad bila ya kuwaongoza waajiri wake kutia kapuni taji la UEFA.

Atletico Madrid ambao waliwabandua mabingwa watetezi Liverpool, watakutana na RB Leipzig ya Ujerumani kwenye robo-fainali huku Atalanta ya Italia ikivaana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

Kampeni za Europa League ambazo pia ziliahirishwa mnamo Machi 2020 kwa sababu ya janga la corona, zitarejelewa Agosti 7. Man-United watapepetana na LASK ya Austria wakijivunia ushindi wa 5-0 katika mkondo wa kwanza ulioshuhudia Wolves wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Olympiakos nchini Uturuki.

Rangers watasafiri Ujerumani kurudiana na Bayer Leverkusen wakilenga kujinyanyua kutokana na kichapo cha 3-1 katika mkondo wa kwanza nchini Scotland.

Mechi kati ya Inter Milan na Getafe na nyingine kati ya Sevilla na AS Roma ambazo hazikuwa zimechezwa kabisa kabla ya kipute cha Europa League kusitishwa, sasa zitakuwa za mkondo mmoja pekee na zitachezewa nchini Ujerumani. Fainali ambayo ilikuwa imepangiwa kuchezewa mjini Gdasnk, Poland hapo awali, sasa itaandaliwa mjini Cologne mnamo Agosti 21.