Michezo

Pep ammiminia sifa tele mvamizi mwiba Aguero

February 12th, 2018 2 min read

Sergio Aguero (kushoto) asherehekea na wenzake baada ya kufungia Manchester City bao kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza dhidi ya Leicester City uwanjani Etihad mnamo Februari 10, 2018. Picha/AFP

Na AFP

MANCHESTER, UINGEREZA

Kwa Muhtasari:

  • Guardiola amsifu Sergio Aguero kwa kufungia timu yake mabao manne
  • Hadi kufikia sasa, Aguero anajivunia jumla ya mabao 28 ndani ya jezi za Man-City msimu huu
  • Guardiola amewataka vijana wake kutozembea katika michuano yote iliyopo mbele yao

KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola alikuwa mwingi wa sifa kwa nyota Sergio Aguero baada ya mvamizi huyo mzawa wa Argentina kufungia timu hiyo jumla ya mabao manne katika ushindi wa 5-1 dhidi ya Leicester City mnamo Jumamosi uwanjani Etihad.

Winga Raheem Sterling aliwafungulia Man-City ukurasa wa mabao mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Jamie Vardy kusawazishia Leicester dakika ya 39.

Hata hivyo, Aguero aliwarejesha Man-City mchezoni katika kipindi cha pili na kuwawezesha miamba hao wa soka ua Uingereza kujivunia jumla ya mabao 14 kutokana na michuano saba iliyopita ugani Etihad.

Ushindi wa Man-City uliwachochea kufungua mwanya wa alama 20 kati yao na Tottenham Hotspur ambao waliwabamiza Arsenal 1-0 ugani Wembley na kuchupa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa EPL, saa chache kabla ya Liverpool kuvaana na Southampton nao Manchester United kumenyana na Newcastle United uwanjani St James’ Park.

 

Mwiba kwa madifenda

“Aguero kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji bora katika ulimwengu wa soka. Kiwango cha ubora wake kinazidi kuimarika kila uchao. Ni sogora wa haiba kubwa ambaye hana kifani kila anapopata mpira ndani ya msambamba wa wapinzani,” akasema Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Kulingana naye, mchuano huo ulikuwa moja kati ya mechi nzuri na za kuridhisha zaidi ambazo zimewahi kusakatwa na Man-City tangu apokezwe mikoba ya kikosi hicho.

Licha ya ushindi huo mnono, Guardiola amewataka vijana wake kutozembea katika michuano yote iliyopo mbele yao huku akiwasisitizia umuhimu wa kutia kapuni mataji mengine zaidi katika kampeni za msimu huu.

Huku wakiwa pua na mdomo na ufanisi wa kujinyakulia ubingwa wa EPL, Man-City huenda wakatia kibindoni ubingwa wa League Cup majuma mawili yajayo wakati watakaposhuka dimbani kunyanyua na Arsenal kwenye fainali.

 

Mabao 21 EPL

Hadi kufikia sasa, Aguero anajivunia jumla ya mabao 28 ndani ya jezi za Man-City msimu huu na magoli 21 ambayo ameyafunga katika EPL ni idadi inayomweka katika nafasi ya tatu nyuma ya Harry Kane na Mohammed Salah kwenye orodha ya wafungaji bora wa EPL.

Kocha Claude Puel wa Leicester alimleta uwanjani kiungo Riyad Mahrez katika kipindi cha pili katika mechi ambayo ilikuwa ya kwanza kwa nyota huyo kuchezea waajiri wake tangu mpango wake wa kuhamia Man-City kuambulia pakavu mwishoni mwa Januari 2018.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi): Tottenham 1-0 Arsenal, Everton 3-1 Palace, Swansea 1-0 Burnley, Stoke City 1-1 Brighton, West Ham 2-0 Watford, Man-City 5-1 Leicester