Pep ataka Manchester City wawe katili zaidi licha ya kuwafagia M’glabach 2-0 kwenye mkondo wa kwanza wa 16-bora UEFA

Pep ataka Manchester City wawe katili zaidi licha ya kuwafagia M’glabach 2-0 kwenye mkondo wa kwanza wa 16-bora UEFA

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amewataka masogora wake kuwa katili zaidi mbele ya malango ya wapinzani licha ya kikosi hicho kupepeta Borussia Monchengladbach ya Ujerumani 2-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumatano usiku.

Ushindi kwa Man-City katika mechi hiyo iliyochezewa jijini Budapest, Hungary, ulikuwa wa 19 mfululizo kwa wanasoka wa Guardiola kusajili kufikia sasa kwenye kampeni za msimu huu wa 2020-21.

Man-City wanaopigiwa upatu wa kutia kapuni taji la UEFA kwa mara ya kwanza msimu huu, walipoteza nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo zingewapa mabao kupitia Bernardo Silva na Gabriel Jesus.

“Tulitamalaki mchuano japo hatukuwa na kiu ya kutaka kufunga idadi kubwa ya mabao. Hilo ni jambo ambalo tuna ulazima wa kubadilisha kikosini haraka iwezekanavyo. Inatubidi tuanze kuwa wepesi wa kutikisa nyavu za wapinzani wetu,” akasema Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Silva alishirikiana na Joao Cancelo kabla ya kufungia waajiri wake bao la kwanza katika dakika ya 29 kabla ya Gabriel Jesus kupachika la pili kunako dakika ya 65.

Hii ni mara ya kwanza kwa Gladbach kutinga hatua ya 16-bora ya UEFA baada ya miaka 43. Man-City watakuwa wenyeji wa mchuano wa mkondo wa pili uwanjani Etihad, Uingereza mnamo Machi 16.

Kiungo Kevin de Bruyne alilazimika kusugua benchi ya Man-City huku mshambuliaji Sergio Aguero akiletwa uwanjani katika dakika za mwisho kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje katika jumla ya mechi 14 za awali.

Kufikia sasa, Man-City wameshinda michuano 42 kati ya 43 ambayo imeshuhudia Gabriel Jesus akicheka na nyavu za wapinzani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Real Madrid yavuna ushindi mwembamba dhidi ya Atalanta...

Spurs watinga hatua ya 16-bora ya Europa League baada ya...