Michezo

Pep awaonya City watarajie mtihani mgumu msimu ujao

May 15th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amebashiri kwamba msimu ujao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) utakuwa mgumu zaidi kuliko uliomalizika mwishoni mwa wiki.

Mkufunzi huyo aliwataka wachezaji wake wajitahidi zaidi kwa vile kila timu itakuwa ikiwalenga kama mabingwa watetezi.

“Nina hakika msimu ujao utakuwa mgumu zaidi, hivyo tutatakiwa kuzidisha juhudi zetu kuliko msimu uliopita,” alisema Mhispania huyo.

“Ni vigumu kuamini kwamba mwaka uliopita (2018) ulipomalizika, Liverpool walikuwa kileleni kwa mwanya wa pointi tisa mbele yetu,,” aliongeza kocha huyo wa zamani wa timu za Barcelona na Bayern Munich.

Kwa kufanikiwa kutwaa taji hilo, Man City imekuwa klabu ya kwanza kutetea ubingwa wake tangu msimu wa 2008-09 wakati Manchester United walifanikiwa kufanya hivyo.

Kwa mara nyingine, historia inaonekana kutokuwa upande wa Liverpool baada ya klabu hiyo kuandamwa na mikasa ya kushindwa kutwaa ubingwa huo dakika ya mwisho

Limekuwa jambo la kawaida kwa timu inayoongoza msimamo wa ligi hiyo wakati wa msimu wa Siku Kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya kuibuka mabingwa, lakini Liverpool imekuwa na mkosi kila inapokaribia kabisa kulitwaa.

Wakati huu, mashabiki wao wengi hawajaamini baada ya vijana hao wa kocha Jurgen Klopp kupoteza ubingwa huo kwa pointi moja tu, na kuwazidishia uchungu mashabiki hao ambao waliufurahia ushindi kwa mara ya mwisho miaka 29 iliyopita (mnamo Aprili 28, 1990).

Katika misimu 11 iliyopita, ubingwa wa ligi hii ulinyakuliwa na klabu iliyokuwa ikiongoza wakati wa misimu hiyo iliyotajwa mara nane, na kati ya mara tatu pekee ambazo haikuwa hivyo- 2008-09, 2013-14 na 2018-19 ni Liverpool ndiyo ilikuwa usukani.

Mambo yamekuwa yakiwaendea vibaya vigogo hao wa Anfield huku mashabiki wao wakiendelea kusubiri taji hilo nyumbani tangu 1990, wakati huo dunia ikiwa na watu 5.2 bilioni, ikilinganishwa na idadi ya sasa ya watu 7.3 bilioni.

Hii ni sawa na kusema watu bilioni 2 hawakuwa wamezaliwa mara ya mwisho waliposhinda ubingwa huo.

Kwenye kikosi cha sasa cha timu hiyo cha wachezaji 27, ni wachezaji watano pekee ambao walikuwa hai wakati timu yao ilitwaa ubingwa huo kwa mara ya mwisho.
Wachezaji hao ni James Milner aliyekuwa na umri wa miaka minne, Adam Lallan na Simon Mignolet walikuwa na umri wa miaka miwili kila mmoja, huku Daniel Sturridge na Dejan Lovren wakiwa na umri wa mwaka mmoja kila mmoja.

Nahodha wa sasa wa klabu hiyo, Jordan Henderson alizaliwa miezi miwili baada ya mwaka huo (1990), wakati Waziri Mkuu akiwa Bi Margaret Thatcher, na mpaka sasa Uingereza imeshakuwa na Mawaziri Wakuu watano.

Rais wa Kenya wakati huo alikuwa Daniel Arap Moi ambaye aliridhiwa na Mwai Kibaki na sasa Uhuru Kenyatta ambaye amebakisha miaka miwili uongozini.

Zilipokutana Januari 3, 2019, Liverpool ilikuwa ikiongoza ligi kwa pointi saba mbele ya City, lakini ikapoteza mechi hiyo kwa 2-1 na kufanya pengo hilo kupunguka hadi pointi nne.

Ilipofika Januari 29, walihitaji ushindi dhidi ya Newcastle United, lakini wakafungwa 2-1 kabla ya kuagana 1-1 na Leicester City na baadaye ikatoka sare 1-1 na West Ham United na kufanya joto liendelee kupanda wachezaji pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

City waliendelea kujiongeza matumaini kufuatia ushindi wao mkubwa wa 6-0 dhidi ya Chelsea ambapo kufikia mechi 27, tofauti ilikuwa pointi moja tu.

Matuamini ya City yaliongezeka zaidi baada ya Liverpool kutofungana na majirani zao, Everton, siku moja kabla ya City kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Bournemoth.

Kuanzia hapo, City waliendelea kushikilia usukani kwa tofauti ya pointi moja hadi walipopewa taji Jumapili kufuatia ushindi wao wa 4-1 dhidi ya Brighton ugenini.