Michezo

Pep Guardiola alia masihara licha ya ushindi

February 22nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

GELSENKIRCHEN, Ujerumani

PEP Guardiola anaamini kuwa Manchester City haitaenda mbali katika kipute cha Klabu Bingwa Ulaya msimu huu isipojifunza kutokana na ushindi wake wa mabao 3-2 dhidi ya Schalke ambapo ilimaliza mechi hiyo na wachezaji 10 siku ya Jumatano usiku.

“Sioni tukienda mbali katika mashindano haya tusipoimarika,” alisema kocha huyu wa City.
“Mwishowe, kujituma kwa (Leroy) Sane na (Raheem) Sterling ndiko kulileta tofauti katika mchuano huu.
“Matokeo haya ni mazuri, ingawa tulipeana penalti mbili na pia kuonyeshwa kadi moja nyekundu. Kwa hivyo hatuko makini sana kupigania taji la Klabu Bingwa Ulaya.”
City ilikuwa mashakani ilipojipata chini mabao 2-1 zikisalia dakika 22 kipenga cha mwisho kilie wakati Nicolas Otamendi alilishwa kadi nyekundu kabla ya mabao kutoka kwa Sane na Sterling katika dakika tano za mwisho kuiwezesha kushinda mchuano huo wa raundi ya 16-bora.
Schalke iliongoza dakika 45 za kwanza 2-1 ikinufaika mara mbili kupata penalti kupitia teknolojia ya kuangalia matukio ya uwanjani kwenye video (VAR), ambazo Nabil Bentaleb alifunga baada ya Sergio Aguero kufungua akaunti ya magoli mjini Gelsenkirchen.

Sane, ambaye alianza kutumiwa dakika 12 za mwisho, alipachika frikiki safi iliyofanya mabao kuwa 2-2 na hakuficha furaha yake kupata bao dhidi ya waajiri hao wake wa zamani.

“Nilitaka kuvuta shuti kutoka mahali hapo kwa sababu nimewahi kupata bao sehemu sawa na hiyo na bao hilo lilitufanya tujiamini na kutupa msukumo wa kushinda,” alisema Mjerumani huyu aliyejiunga na City mwaka 2016 akitokea Schalke.

“Hatukuwa na mwanzo mzuri, lakini nafurahia tulipata ushindi na kufunga mabao matatu ugenini, hiyo ni hatua muhimu sana.”

City bado ina kazi kubwa ya kufanya katika mechi ya marudiano Machi 12 uwanjani Etihad, huku Fernandinho, ambaye alionyeshwa kadi ya njano akisababisha penalti na Otamendi wote wakitumikia marufuku.

Licha ya mechi kusimamishwa kwa dakika tatu baada ya hitilafu ya kimitambo kuchelewesha refa Carlos del Cerro Grande kutoa uamuzi kuhusu Otamendi kunawa mpira ndani ya kisanduku, Guardiola alisema yeye ni shabiki wa VAR.

“VAR inahitaji muda, wahusika waitaimarika, skrini ilikuwa imevunjika, watakuwa bora wakati ujao,” alisema Guardiola.

“Naunga mkono teknolojia hii kwa sababu marefa wanahitaji usaidizi.”

Kilichomkera Guardiola sana kuhusu mchezo wa vijana wake ni kufungwa mabao mawili licha ya kuwa Schalke ililenga goli mara mbili katika dakika 90.

Wachezaji wa Schalke 04 kabla ya kucheza dhidi ya Manchester City. Picha/ AFP

“Walilenga goli mara chache sana na walipata mabao mawili kwa hivyo bado tuna kibarua kikubwa,” alisema Mhispania huyo.

“Ninaonea fahari kuenda ugenini na kupata mabao matatu, lakini hilo halitoshi katika kiwango hiki.

“Tuliwapa nafasi za kutawala mechini na hatuna budi kuimarisha mchezo wetu.”

Kwa jumla, Guardiola alikuwa na cha kujivunia zaidi kuliko kulalamika kutokana na ushindi huo wa dakika ya mwisho.

Baada ya kuwaongoza viongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza na hata kukaribia kupata ushindi wa kihistoria kwenye Klabu Bingwa Ulaya, kocha wa Schalke, Domenico Tedesco alisikitika mno.

“Kichapo cha mabao 3-2 bila shaka kinasikitisha,” alisema Tedesco, ambaye vijana wake wako karibu na maeneo hatari ya kutemwa kutoka Ligi Kuu ya Ujerumani katika nafasi ya 14.