Makala

Pepo wa uvutaji bangi, unenguaji viuno atua Murang’a

January 4th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MUUNGANO wa viongozi wa dini asili na wenzao wa kitamaduni wametoa malalamiko kuhusu mtindo wa baadhi ya baa katika kaunti hiyo kuandaa hafla za vijana kushindana kuvuta bangi huku nao wanawake wakishindana kunengua viuno ambapo inadaiwa baadhi huingia jukwaani wakiwa uchi wa mnyama.

Wanalalama kwamba serikali imekaa kimya huku pepo wa bangi na uanikaji uchi akivuma ndani ya baa na kupewa hifadhi kinyume na maadili ya kiroho na ya kitamaduni.

Katika taarifa ya pamoja ya Januari 2, 2024, ikiwa na saini za wachungaji sita na wazee wa kitamaduni watatu, walisema kwamba maovu hayo ni ushahidi wa utepetevu wa vyombo vya kudumisha usalama lakini pia hujuma kwa jitihada za Naibu Rais Rigathi Gachagua za kupambana na mihadarati na utundu ndani ya baa.

“Visa vya walanguzi wa mihadarati kuhamia ndani ya baa ambapo hutenga nafasi za uuzaji na uvutaji bangi vimechipuka kwa ujasiri mkuu, baadhi ya polisi wakihusika kufanikisha visa hivyo,” ikasema ripoti hiyo.

Madai hayo yanawiana na yale ambayo Mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua alitoa hivi majuzi akisema baadhi ya maafisa wa polisi katika eneobunge hilo ni washirika wa ulanguzi wa bangi hasa katika mitaa ya Kiambamba.

Mnamo Desemba 30, 2023, Kamanda wa polisi wa wadi ya Township Bw Patrick Lumumba aliongoza kikosi cha wadogo wake kuvamia baa moja iliyoko mjini Murang’a na ambapo baadhi ya wateja walikuwa wakivuta bangi hadharani wakiketi na kubugia pombe.

Glasi za bia. PICHA | MAKTABA

Kabla ya maafisa hao kufika, habari za msako huo zilikuwa zimefikia wasimamizi wa baa hiyo ambao waliwaonya wavutaji bangi hao wahepe.

“Nimekuwa nikiambia ninyi kwamba kuna mambo ambayo hayaeleweki ambayo hutendeka ndani ya hii baa. Natoa onyo kali kwamba iwapo tutanasa washukiwa wakishiriki uvutaji ndani ya hii baa wa kukamatwa kwanza watakuwa wamiliki, wasimamizi na wahudumu kabla hata ya sisi kuwafunga pingu wauzaji na wavutaji,” Bw Lumumba akarekodiwa akionya.

Wenyeji tayari wametoa makataa ya kuandaa maandamano iwapo walanguzi na wavutaji bangi hawatazimwa eneo hilo la makazi ambapo Katibu wa Wizara ya Uchumi wa Baharini na Madini Bw Elijah Mwangi, humiliki jumba la upangaji.

Aidha, walilalama kuwa eneo hilo huwa na steji kuu ya kuelekea Kaunti za Kirinyaga na Nyeri hivyo basi kutumiwa na watoto wa shule na ambao wanaweza wakageuzwa kuwa wateja wa mihadarati.

Taarifa hiyo ilisema kwamba kuna baa kadha za Murang’a ambazo zinawasajili hata wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 na ambao ni wanafunzi, kunengulia walevi viuno wakiwa uchi na kuwalipa kupitia pombe na kuwapa wanaume wa kushiriki ngono nao kwa malipo.

Walisema kwamba baa hizo humilikiwa na mabwanyenye, wanasiasa na nyingine zikiwa ni za maafisa wa usalama.

Mnamo Oktoba 2023, kulitekelezwa msako katika mji wa Murang’a ndani ya baa moja na kukanaswa wasichana watatu wa umri mdogo waliokuwa wakishirikishwa ngoma bila nguo huku wanaume wengine rika la akina baba na akina babu zao wakishangilia.

“Hata tukilalamika kwa kamati za usalama ya kaunti, hakuna lolote ambalo hufanyika kwa kuwa taasisi nyingi eneo hili zimetekwa nyara na ukwasi, ushawishi na kutojali kutoka kwa washirikishi wa maovu hayo kwa jamii.

Waliteta kwamba “katika siku za hivi punde tumeshuhudia visa vya wazi vya wakuu wa kiusalama kupuuza tetesi hata zinazohusu watoto na maeneo yao ya elimu na makazi ambapo kelele za mabaa usiku kucha huathiri haki zao za amani ndani ya malezi”.

Walimtaka Kamishna wa Kaunti Patrick Mukuria kuwajibikia kero hizo wakisema kwamba “mtangulizi wako Bw Karuku Ngumo alikuwa akishughulikia tetesi zetu kuhusu kero hizi za kusambaratika kwa maadili lakini katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia kutojali na kutowajibika”.

Mnamo Desemba 9, 2023, Bw Mukuria akihutubu katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ufisadi Duniani, alikiri kwamba “ulevi ni janga moja kuu linalotukabili hata ndani ya huduma kwa umma kiasi cha kutatiza utawala”.